1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sweden yatinga nusu fainali kandanda la wanawake Ulaya

23 Julai 2022

Timu ya taifa ya wanawake ya Sweden imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kandanda la wanawake barani Ulaya Euro 2022 baada ya kuibamiza Ubelgiji bao 1-0 usiku wa kuamkia Jumamosi.

Fußball | Frauen EM 2022 | Sweden v Portugal: Group C
Picha: Naomi Baker/Getty Images


Wakati wa mchezo huo wa tatu wa robo fainali bao lililofungwa na mlinzi wa timu hiyo ya Sweden Linda Sembrant ndiyo liliitoa kimasomaso nchi hiyo na kuiwezesha kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali.

Ubelgiji ilitumia mchezo wa kuvizia ikiwadhibiti Sweden wakati wa vipindi vyote viwili huku ikitumia nafasi za hapa na pale kufanya mashambulizi. Ilitazamiwa kwa aina hiyo ya mchezo Ubelgiji pembeni ingelazimisha kuupeleka mtanange huo hadi katika dakika za nyongeza. 

Hata hivyo inaonesha mpango huo haukufua dafu. Jaribio la mwisho miongoni mwa nafasi 34 ilizopata Sweden kwenye lango la Ubelgiji lilitosha kumwezesha Sembrant kupachika wavuni bao safi kabisa na kuzima ndogo za Ubelgiji kucheza nusu fainali.

"Hatukutaraji kuingia dakika za nyongeza " amesema Sembrant alipozungumza na kituo cha utangazaji cha SVT, akiongeza kwamba timu yake ilifanikiwa kuwaendesha puta Ubelgiji lakini kilichokosekana kwa muda mrefu ilikuwa goli.

Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Sweden Picha: Naomi Baker/Getty Images

Na hatimaye likapatikana wakati wa dakika ya pili miongoni mwa zilizoongezwa na mwamuzi baada ya dakika 90 kukamilika. Fursa hiyo ilitokana na mpira wa kona uliochongwa vizuri na mshambuliaji Asllani na kutua katikati mwa eneo la 18.

Aliyeugusa mwanzo alikuwa Nathalie Bjorn lakini shuti lake liliwekewa kigingi na hapo ndiyo Sembrant akachangamsha miguu kwa shuti jingine lililotikisa nyavu za Ubelgiji.

Nani kukabana koo na nani hatua ya nusu fainali? 

Kwa ushindi huo Sweden itateremka dimbani kupambana na wenyeji wa michuano hiyo ya EURO 2022 timu ya taifa ya wanawake ya England katika mchezo wa nusu fainali wiki inayokuja.

England ilifuzu kucheza nusu fainali ya mashindano hayo ilipoibamiza Uhispania magoli 2-1 Jumatano usiku. Hii ni mara ya nne kwa timu ya soka ya England upande wa wanawake kufuzu kwa mechi ya nusu fainali lakini hawajawahi kutawazwa mabingwa wa Ulaya.

Time nyingine iliyotangulia nusu fainali ni Ujerumani. Timu hiyo ya taifa ya wanawake ilijisafishia njia kwa kuitandika mabao mawili kwa nunge timu ya taifa ya wanawake ya Austria.

Ujerumani ilipoteremka dimbani dhidi ya Austria. Mchezo ulimalizika kwa Ujerumani kuishinda Austria 2-0.Picha: Dylan Martinez/REUTERS

Mchezo huo wa Alhamisi usiku ulisadifu kuwa mgumu kwa Ujerumani lakini ulimalizika kwa kuiwezesha nchi hiyo kusonga mbele katika kampeni yake ya kulitwaa kombe kandanda la wanawake barani Ulaya kwa mara ya tisa.

Ujerumani itacheza nusu fainali baada ya kupita kwenye tanuri la moto baada ya hatua ngumu ya makundi. Kundi la Ujerumani lilizijumuisha timu nyingine vigogo za Denmark, Uhispania na Finland.

Hii leo unasubiriwa mchezo wa mwisho wa robo fainali utakaoamua ni nani atakipiga na Ujerumani kwenye mchezo wa nusu fainali kati ya Uholanzi au Ufaransa.

Mchezo huo utakaopigwa huko Yorkshire Kusini utatoa picha halisi ya awali ya jinsi nusu fainali itakavyokuwa na hata utabiri wa mapema wa fainali ya kandanda la wanawake barani ulaya mwaka huu 2022.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW