1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria; Makubaliano huenda yakafikiwa

24 Oktoba 2012

Mjumbe wa kimataifa nchini Syria Lakhdar Brahimi amedokeza leo(24.10.2012)kuwa pande zinazohusika katika mzozo nchini Syria huenda zikakubaliana kusitisha mapigano katika wakati wa sikukuu ya Waislamu ya Idd el Hajj.

epa03440917 A handout picture released by the Syrian Arab news agency SANA shows Syrian president Bashar Assad (L) receiving the joint UN and Arab League peace envoy Lakhdar Brahimi (C) and Syrian Deputy Foreign Minister Faysal Al Mokdad (R) at the presidential palace in Damascus, Syria, 21 October 2012. EPA/SANA HANDOUT EDITORIAL USE ONLY/NO SALES
Rais Assad akikutana na Brahimi mjini DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo mamia ya wakimbizi kutoka Syria wameingia katika kambi ya muda ya wakimbizi karibu na mpaka wa Uturuki, wakikimbia kile walichosema kuwa ni wiki ya mashambulizi makali ya jeshi la serikali tangu kuanza kwa vuguvugu la uasi miezi 19 iliyopita.

Akizungumza mjini Cairo, mjumbe wa kimataifa wa amani nchini Syria Lakhdar Brahimi amesema kuwa pande zinazohusika katika mzozo nchini Syria huenda zikakubaliana kimsingi kusitisha mapigano.

Brahimi amesema kuwa pande zinazohusika zitatangaza makubaliano hayo baadaye. Ameongeza kuwa iwapo makubaliano hayo yatafikiwa ,yatasafisha njia kwa makubaliano imara zaidi ya kusitisha mapigano na kuelekeza katika hatua za kisiasa.

Baraza la usalama

Mjumbe huyo wa kimataifa wa amani nchini Syria atalihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa njia ya video kutoka Cairo, kwa mujibu wa msemaji wa umoja wa mataifa Martin Nesirky.

"Brahimi anajitahidi kwa uwezo wote alionao, kama anavyofanya katibu mkuu, kwa kuwa huu ni wakati muhimu sana," Nesirky amewaambia waandishi habari mjini New York.

Brahimi amekutana na rais Bashar al-Assad siku ya Jumapili wakati wa ziara yake ya siku tano nchini Syria katika azma ya kujaribu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya majeshi ya serikali na waasi katika muda wa siku nne za sikukuu ya Eid al-Adha, ambayo inaanza Ijumaa.

Kofi Annan , mtangulizi wa Brahimi katika usuluhishi wa mzozo huu, alijitoa kutoka ujumbe huo mwezi August, akilaumu mgawanyiko uliopo katika baraza la usalama la umoja wa mataifa na kushindwa kwa serikali ya Syria kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo hayakuwezekana.

Brahimi anatarajiwa kukutana leo(24.10.2012) mjini Cairo na katibu mkuu wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu , Arab League Nabil al-Arabi kwa mazungumzo kuhusiana na mzozo huo uliodumu sasa miezi 20.

Katibu mkuu wa Arab League Nabil al-ArabiPicha: picture-alliance/dpa

Mapigano yanaendelea

Nchini Syria kwenyewe , majeshi ya serikali yameongeza mashambulizi yake katika jimbo la kaskazini la Idlib wakiwania kuudhibiti tena mji muhimu uliotekwa na waasi wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la uchunguzi wa haki za binadamu nchini Syria , kiasi ya watu 190 wameuwawa jana nchini humo ikiwa ni pamoja na watu 77 waliouwawa katika maeneo ya vitongoji vya nje ya mji mkuu Damascus.

Shambulio la bomu katika mji wa DamascusPicha: Reuters

Wakati huo huo mamia ya wakimbizi wamemiminika katika kambi ya muda ya wakimbizi karibu na mpaka na Uturuki , wakikimbia kile walichosema kuwa ni mashambulio makubwa ya makombora ya jeshi ya Syria tangu vuguvugu hilo la uasi kuanza miezi 19 iliyopita.

Katika muda wa siku mbili zilizopita , mahema 700 yamewekwa katika eneo kubwa la shamba la mizaituni katika eneo la milima ndani ya Syria na wakimbizi wote wameorodheshwa.

Familia kadha ambazo hazina makaazi zimeingia katika kambi hiyo na kujikuta hazina nafasi ya kujihifadhi, lakini wanahofu ya kurejea katika makaazi yao kutokana na hali mbaya ya mashambulizi ya mfululizo ya kila siku.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / rtre

Mhariri :Hamidou Oummilkheir

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW