1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na Kasheshe ya ndege bila ya rubani magazetini

21 Mei 2013

Hali nchini Syria,kishindo cha ndege inayorushwa bila ya rubani na kashfa ya kupendeleana katika chama cha CSU ni miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani.

Mtaa wa Deir al Zor umeteketezwa kutokana na mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi May 15 mwaka huuPicha: Reuters

Tuanzie lakini na Mashariki ya kati ambako damu inazidi kumwagika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.Gazeti la Nordwest-Zeitung linaandika:"Kila kukicha mapigano yanazidi kuwa yakikatili.Madola makuu,Marekani na Urusi hayakupata la maana badala ya kuitisha mkutano wa kimataifa.Serikali ya Obama na wanamikakati wa Kremlin wanatambua fika:ufumbuzi wa amani umepitwa na wakati.Jumuia ya kimataifa imeipoteza fursa ya kuzinyamazisha silaha.Mustakbal wa Syria si mzuri:Inamaanisha watu wengi zaidi watalazimika kuihama nchi yao,mapigano yatazidi makali na kutishia kuenea katika nchi nyengine.Balaa haliko mbali kutokea katika eneo hilo."

Gazeti la "Straubinger Tagblatt/Landshuter linazungumzia jinsi hali ilivyobadilika katika uwanja wa mapigano na kuandika."Si muda mrefu uliopita, walimwengu waliashiria mwisho wa enzi ya rais wa Syria Bashar al Assad hauko mbali.Ama angekimbilia uhamishoni katika nchi rafiki au wapinzani wake wangemteka nyara.Mradi asingeitawala tena Syria.Hii leo lakini mambo yamebadilika hatima ya enzi yake iko mbali zaidi kuliko wakati wowote ule tangu malalamiko dhidi yake yalipoanza miaka miwili iliyopita.Kwamba wapinzani hawako mbali kuibuka na ushindi,hoja hizo hakuna tena anaezizungumzia."

Thomas de Maizière abanwa

Mada ya pili iliyogonga vichwa vya habari inahusu kishindo kinachomtikisa waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière kuhusu mradi wa kutengenezwa ndege isiyokuwa na rubani Euro Hawk.Koti la waziri limeingia dowa linaandika gazeti la "Reutlinger General Anzeiger" na kuendelea:"Kwa jumla Thomas de Maizière anatajikana kuwa mwanasiasa makini na mwenye kuaminika.Lakini hivi sasa analazimika kujieleza.Mapema mwezi ujao anapanga waziri huyo kujibu masuala ya kamati maalum ya bunge.Itakuwa vizuri ikiwa majibu yatakuwa mengi zaidi.Lakini kama hiyo itakuwa dawa,hakuna ajuaye kwasababu kishindo cha kisiasa cha kadhia hiyo ya ndege isiokuwa na rubani kimeanza tangu mwaka 2001-wakati ule waziri wa ulinzi alikuwa Rudolf Scharping wa chama cha SPD.Wakuu watano tofauti walihusika na mradi huo tangu wakati huo.Katika kipindi cha zaidi ya mwongo mmoja mawaziri kadhaa wamejikwaa katika mradi huo unaoonyesha kuacha njia.De Maiziere anaweza pia kuteleza muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu."

Waziri wa ulinzi Thomas de Maiziere amepiga picha karibu na sanamu la ndege inayoruka bila ya rubani ya Euro Hawk katika kituo kimoja karibu na BonnPicha: Reuters

Kshfa ya kupendeleana yafichuliwa Bavaria

Mwenyekiti wa chama cha CSU na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst SeehoferPicha: picture-alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho inahusu kasheshe ya kupendeleana wanasiasa wa chama kidogo cha CSU na familia zao katika jimbo la kusini la Bavaria.Gazeti la "Münchner Merkur" linaandika."Seehofer hana njia nyengine.Lazma awaachishe kazi wanachama watatu wa serikali yake kutoka chama cha CSU waliowapatia kazi jamaa zao muda mfupi kabla ya kuanza kufanya kazi sheria inayopiga marufuku mitindo ya kupendeleana kazini.Akishindwa kufanya hivyo,madhara yake yatamrejea yeye mwenyewe.Amempokonya wadhifa wake mkuu wa kundi la chama cha CSU katika bunge la jimbo hilo la kusini na kumlazimisha waziri arejeshe fedha alizopokea za kuihudumia familia.Hatua mpya zilizochukuliwa zinamlazimisha Seehofer kuwajibika kwa mara nyengine tena.Mkuu huyo wa chama cha CSU anazongwa na kizungumkuti:Akichukua hatua basi atajitafutia maadui wengine wakubwa chamani.Akiachilia mbali,wapiga kura watamgeukia."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW