1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na kitabu cha James Comey magazetini

Oumilkheir Hamidou
17 Aprili 2018

Mzozo wa Syria na kitabu cha mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi wa ndani nchini Marekani FBI, James Comey ni miongoni mwa mada zilizogubika magazeti ya Ujerumani hii leo.

Syrien Raketenangriff
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

 

Tunaanzia Syria ambako wahariri wanajiuliza kama kweli juhudi mpya za kusaka ufumbuzi wa amani baada ya hujuma za kijeshi za jumamosi iliyopita, zitaleta tija. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika: "Miito ya kuanzishwa juhudi mpya za amani inatajwa kuwa haina maana. Baraza la usalama la umoja wa mataifa limegawika, juhudi za mpatanishi maalum wa Umoja wa Mataifa tangu mwanzo zilikuwa kazi bure. Sasa kwanini  hali iwe tofauti hivi sasa, eti tu kwasababu rais wa Ufaransa anataka kujigeuza mshika bendera. Ukweli  ambao ni mchungu ni kwamba malumbano yamempatia tija tangu Assad mpaka Putin. Wakitaka kuibadilisha hali ya mambo, nchi za magharibi zitalazimika kujitwika mzigo mzito na hasa tangu Trump kuifanya iyumbe yumbe jumuia ya kujihami ya NATO.Tatizo ni kwamba hakuna anaeweza kuashiria mzigo huo utakuwa wa aina gani?"

Uamuzi wa busara wa Ujerumani

Baada ya Iraq na Libya, na safari hii pia serikali ya Ujerumani imeamua kutojiunga na hujuma za kijeshi za washirika wa jumuia ya kujihami ya NATO. Mhariri  wa gazeti la "Neue Osnabrücker" anajiuliza kama msimamo huo unaweza kuipatia Ujerumani imani ya pande zinazohusika na kukubalika kama mpatanishi. Gazeti la "Neue Osnabrücker linaendelea kuandika: "Katika siasa ya nje watu wanabidi wazingatie hali halisi namna ilivyo: Katika kadhia ya Syria mtazamo wa serikali kuu ya Ujerumani umekawia sana. Ikiwa Berlin sasa inakiri, Bashar al Assad anabidi ajumuishwe katika juhudi za kusaka ufumbuzi wa amani, ni sawa. Vyenginevyo isingewezekana na Urusi haitokubali ufumbuzi wowote bila ya kushirikishwa Assad. Ikiwa wananchi wa Syria watapata amani wanayoihitaji na nchi hiyo kujipatia matumaini ya kuchipuka upya, basi kuwepo Assad madarakani, itakuwa sawa na nusu shari katika juhudi za ufumbuzi wa vita vya nyanja tofauti nchini humo."

Kitabu cha James Comey chafichua mengi

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka Marekani ambako mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi wa ndani FBI, Jamey Comey amechapisha kitabu akifichua mengi dhidi ya rais wa Marekani Donald Trump. Mhariri wa gazeti la "Oberhessischen Presse" anajiuliza kama kuna litakalotokea baada ya Comey kuchapisha kitabu chake."Hakuna chochote kitakachotokea. Hata mwenyewe Comey haamini kama yaliyofichuliwa ndani ya kitabu hicho yatapelekea kuanzishwa utaratibu wa kumpokonya Trump madaraka. Hasha, Comey analenga zaidi ufafanuzi na kutaraji kwamba wapiga kura, kutokana na kufichuliwa ripoti hizo zinazotisha watatanabahi na kumgeukia Donald Trump ili kufungua njia ya mageuzi ya kisiasa, uchaguzi utakapoitishwa nchini humo. Msimamo huo haulingani lakini na Comey, mtu aliyekuwa akiongoza idara ya upelelezi wa taifa na ambae kimsingi anazijua chini juu sheria na mwongozo wa Marekani. Lakini pengine ameamua kufanya hivyo kwasababu haamini kama mpelelezi maalum Robert Müller atafanikiwa kweli kumfikisha Trump mahakamani."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW