Mapinduzi yaliokwapuliwa Syria
15 Machi 2017Huko Bahrain familia ya Al-khalifa bado inatawala. Nchini Libya baada ya kun´golewa madarakani Gaddafi nchi hiyo imeingia katika machafuko. Lakini yote hayo yamegubikwa na hali ya mambo nchini Syria. Kile kilichoanza kama maandamano ya amani Machi 2011 sasa kimepamba moto na kugeuka vita vya kikatili ambavyo vimedumu muda mrefu kuliko vita vya pili vya dunia.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hivi sasa zaidi ya watu 400,000 wamegeuka wahanga wa vita hivyo. Mgogoro huo umesababisha wimbi kubwa la wakimbizi la wakati huu. Zaidi ya nusu ya wakaazi wapatao milioni 21 wa Syria wameyakimbia makaazi yao.
Mjini Geneva, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu Seid raad al-Hussein amesema wiki hii kwamba mzozo wa Syria ni janga kubwa kabisa la binaadamu tangu vita vya pili vya dunia. Nchi hiyo imegeuka kuwa ukumbi wa mateso.
Mauwaji dhidi ya raia
Mtawala Bashar al-Assad kama alivyokuwa baba yake Hafidh al-Assad analitumia jeshi kuwashambulia na kuwauwa raia wake mwenyewe kwa mabomu au kama asemavyo mtaalamu kuhusu Syria katika taasisi ya Carnegie inayohusika na Mashariki ya kati Yezid Sayigh, " baba na mtoto wamedhihirisha nia zao katika kutumia nguvu kupita kiasi.”
Mtazamo usiowa kawaida wa hali nchini Syria ulifafanuliwa na Makamu wa zamani wa rais wa Marekani Joe Biden katika mhadhara kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Harvard Oktoba 2, mwaka 2014. Wakati wa maswali na majibu kwenye mhadhara huo wa dakika 52, Biden alisema, " Washirka wetu ndiyo tatizo letu kubwa nchini Syria. Uturuki, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu-wote lengo lao kubwa likuwa ni kumuangusha Assad na kusababisha vita baina ya Wasunni na Washia huku zikimimina mamilioni ya dola na tani elfu kadhaa za silaha kwa kila mmoja wao-Al Nusra na Al-Qaeda pamoja na wapiganaji wa jihadi wa siasa kali kutoka kote duniani.” Biden akawaambia wanafunzi hao, "Msikate tama katika kuisaidia Syria.
Jitihada zilizoshindwa nchini Syria
Lakini kile ambacho Biden hakukisema ni kwamba mpango wa muda mrefu wa Marekani yenyewe kutaka kuleta mabadiliko ya utawala Syria, hata kabla ya mwaka 2011 haukufanya kazi. Kwa mfano ni ujumbe wa shughuli za ubalozi wa Marekani mjini Damascus uliochapishwa na mtandao wa Wikileaks na kufichuwa kwamba afisa wa ubalozi wa marekani mjini Damascus William Roebuck alitamka mnamo Desemba 2006 kwamba wanaamini udhaifu wa Bashar uangaliwe kwa namna anavyochukua hatua wakati wa hatari, kwa mfano kwa kupima mgongano uliopo kati ya mageuzi ya kiuchumi na kitisho kikubwa kwa utawala wake kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wafuasi wa itikadi kali. Katika ujumbe huo huo afisa huyo wa Marekani akapendekeza upaliliwe mzozo kati ya Wasunni na Washia.
Kwa upande mwengine baada ya miaka sita ya vita, Urusi na Iran ndiyo nguvu kubwa nchini Syria. Kwa wanaowaunga mkono wapinzani, mtaalamu Sayigh anasema, Marekani, nchi za Ulaya, Saudi Arabia na Qatar na pia Uturuki tangu katikati ya mwaka jana wanachukua msimamo. Lakini mtaalamu huyo anasema pamoja na kuwa wamejaribu kumaliza vita hivyo, lakini yeye binafsi hatarajii kutapatikana makubaliano rasmi, badala yake utawala wa Assad utaendelea kuweko madarakani.
Huo ni mtazamo wa wachambuzi wengi barani Ulaya. Hata ikiwa vita vitaendelea kwa miaka michache, swali la ujenzi mpya wa Syria ambayo imeharibiwa kwa sehemu kubwa litakuwa zingatio kubwa Na ndiyo maana kuna haja ya uumoja wa Ulaya kujihusisha zaidi katika kutafuta suluhisho, kwani kwa jumla kwa Wasyria unazingatiwa kuwa ni mshirika wa kuaminika sio tu nchini Syria kanda nzima ya Mashariki ya kati. Mchango wa Ulaya usiwe tu katika misaada ya kiutu bali suluhisho la kisiasa. Hilo litakuwa jambo jema kwasababu tatizo la Syria liko moja kwa moja, mlangoni mwa Ulaya.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / von Hein, Matthias, dw
Mhariri: Yusuf Saumu