1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Shughuli ya kuwaondoa wagonjwa waliozingirwa yaanza

27 Desemba 2017

Shughuli za kuwaondoa watu ambao wanahitaji matibabu waliokwama katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi Mashariki ya Ghouta nchini Syria na kuwapeleka Damascus zimeanza.

Syrien Ost-Ghouta Hilfsorganisation
Picha: Reuters/B. Khabieh

Shughuli za kuwaondoa watu ambao wanahitaji matibabu lakini wamekwama katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi Mashariki ya Ghouta nchini Syria na kuwapeleka Damascus zimeanza. Hayo ni kwa mujibu wa kamati ya kimataifa ya shirika la Msalaba Mwekundu. Wakatzi huo huo Urusi imetangaza kurefusha muda wa kambi zake za kijeshi nchini Syria.

Takriban watu 400,000 Mashariki ya Ghouta wamezingirwa na vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad. Umoja wa Mataifa umeisihi serikali kuruhusu shughuli za kuwaondoa wagonjwa 500 wakiwemo watoto wanaougua saratani kupata matibabu.

Chama cha wahudumu wa afya wa Syria na Marekani (SAMS) kimesema wagonjwa wanne walipelekwa hospitalini mjini Damascus, hao wakiwa kati ya wagonjwa 29 walio katika hali mbaya kiafya walioruhusiwa kuondolewa. Waliosalia wataondolewa katika siku zinazofuata.

Wagonjwa kupewa kipaumbele

Wagonjwa wakiwemo watoto ni miongoni mwa waliozingirwa Mashariki ya GhoutaPicha: picture-alliance/AA/A. Damashqy

Wiki iliyopita mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria Jan Egeland alisema katika kikao na waandhishi wa habari mjini Geneva, kwamba mchakato wa mazungumzo umewafelisha watu wengi mwaka huu wa 2017.

"Watu 494 wako katika orodha ya wanaohitaji kupewa kipaumbele kuondolewa kupata matibabu, idadi hiyo inapungua. Si kwa sababu tunawaondoa watu lakini kwa sababu watu wanafariki”.

Meneja anayesimamia utetezi katika shirika la SAMS Mohamad Katoub amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa watano walioidhinishwa kuondolewa ni sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya serikali ya Assad na kundi la waasi la Jaish al-Islam.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Syria limesema shughuli ya kuwaondoa wagonjwa hao ni matokeo ya muda mrefu wa mazungumzo.

Urusi kurefusha muda wa kambi zake za jeshi Syria

Manowari ya Urusi katika kambi ya Tartus nchini SyriaPicha: picture-alliance/epa/SANA

Katika tukio jingine siku ya Jumanne, bunge la Urusi lilipiga kura ya kurefusha muda wa kambi yake ya wanajeshi wa majini iliyoko Tartus na kambi ya wanajeshi wake wa angani iliyoko Hmeimim nchini Syria kwa muda wa miaka 49 zaidi.  Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema hatua hizo zimeshaidhinishwa.

"Wiki iliyopita Amiri Mkuu wa majeshi (Rais Vladimir Putin) alitoa idhini kuhusu muundo na maafisa wa kambi za Tartus na Hmeimim. Tumeanza harakati za uwepo wa kudumu hapo".

Hatua hiyo itaiwezesha Urusi kuwa na manowari 11 katika bahari ya Mediterrania ufuoni mwa Syria vikiwemo vyombo vya kinyuklia.

Mwandishi: John Juma/RTRE/

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW