Umoja wa Mataifa umeshindwa kupata suluhisho ya Syria
6 Julai 2018Urusi ambayo inashiriki kwenye mashambulizi ya angani dhidi ya waasi nchini Syria imesema kukosekana huko kufikiwa muafaka kunatokana na kwamba wakati wajumbe wengine wa Baraza hilo wakilenga kumaliza uhasama, wao Urusi wanalenga kupambana na magaidi.
Vita katika eneo la Daraa, moja ya ngome za mwisho za waasi, karibu na Jordan na Milima ya Golan iliyokaliwa na Israeli, vilianza Juni 19 na vimesababisha karibu watu 330,000 kukimbia makaazi yao. Wanaharakati wa upinzani wanasema kuwa mamia ya watu wameuawa.
Urusi yazuia mwafaka
Balozi wa Urusi katika Braza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Vassily Nebanzia, alisema kuwa Urusi inakubaliana na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la kuwapa misaada ya kibanadamu, lakini sio kwenye mapambano dhidi ya wale aliowaita magaidi, "tuko mbali kuafikiana kwa sababu wao wanalenga kusitisha uhasama, na sisi tunalenga kupigana na waasi. Lakini tunakubaliana kuhusu kusitisha mashambulizi dhidi ya wanaotoa misaada, kwa lengo la kuwasaidia wale ambao wameathirika. Pia tuna tatizo na idadi ya watu ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu."
Balozi wa Sweden katika Umoja wa Mataifa, Olof Skoog, ameitisha mazungumzo ya dharura na Kuwait, mwakilishi wa mataifa ya Kiarabu, akitarajia kuwa atapata uungwaji wa wanachama 15 watakaoafikiana kuhusu kusitishwa kwa uhasama na kurahisisha misafara ya misaada kwa watu wanaohitaji.
Guterres ahuzunishwa na hali Daraa
Skoog alisema kuwa kila mwanachama alielezea wasiwasi kuhusu janga la kibinadamu na mataifa mengi yanaamini kuwa ni suala la dharura kwa mwafaka uliopatikana mwezi Februari kutekelezwa ili kusitisha mashambulizi na misaada kusafirishwa.
Skoog aliwaambia wanahabari kuwa kile anachodhani kwa sasa ni kuwa baadhi ya wanachama wanatofautiana kwa sababu msisitizo kwa sasa ni kule makabiliano yanapofanyika ambapo mataifa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanahusika moja kwa moja.
Aliongeza kusema kuwa anatarajia kuwa Baraza hilo litafanya mkutano mwengine kwa kile alichokitaja kuwa hali inayozidi kuwa mbaya zaidi.
Msemaji wa Umoja huo, Stephane Dujarric, alisema kuwa Katibu Mkuu Antonio Guterres ana wasiwasi mkubwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea kusini magahribi mwa Syria na athari zake kwa raia.
Kwa mara nyingine tena, Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama na kurejelewa kwa mazungumzo, akisisitiza kuwa "maisha ya karibu raia 750,000 yako kwenye hatari," Dujarric alisema.
Mwandishi: Shisia Wasilwa/AP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef