1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yafanya mazungumzo ya amani na makundi ya upinzani

27 Desemba 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kuwa serikali ya Syria inafanya mazungumzo na wapinzani kabla kuanza kwa mazungumzo ya amani yatakayofanyika nchini Kazakhastan mwezi ujao.

Russland Sergei Lawrow in Moskau
Picha: Getty Images/AFP/N. Kolesnikova

Kauli ya Lavrov, hata hivyo, haikutaja wapi mazungumzo hayo yanafanyika na nani hasa wanaoshiriki. Tayari Kamati ya Juu ya majadiliano, HNC, chombo ambacho kinawakutanisha makundi ya wenye silaha pamoja na wanasiasa wanampinga Rais Bashar al-Assad, kimesema kuwa hakina taarifa yoyote kuhusu mazungumzo hayo.

Kamati hiyo pia inayajumuisha makundi ambayo yanampinga Assad chini ya mwamvuli wa Free Syrian Army na ilishiriki katika jitihada za uzinduzi wa mazungumzo ya amani mapema mwaka huu.

Urusi, Iran na Uturuki zimesema kuwa ziko tayari kusadia kusimamia makubaliano ya amani baada ya kufanyika kwa mazungumzo mjini Moscow wiki iliyopita, ambako pia walipitisha azimio la kuweka kanuni za kuzingatia kwa kila makubaliano ya amani.

Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema kuwa nchi zote tatu zimekubaliana, Rais Assad amekubali pia kuwa mazungumzo hayo yafanyike katika mji mkuu wa Kazakhastan.

Marekani na Urusi pia zimeendeleza mazungumzo dhidi ya vita na kundi linalojiita dola la kiislam IS, mazungumzo hayo sasa yameboreshwa na kuwa ya mara kwa mara huku kila upande ukitoa taarifa kwa muda halisi pia kuainisha baadhi ya malengo ya kimkakati kwa miezi kadhaa ijayo.

Katika mazungumzo hayo Urusi imeweka wazi kipaumbele chake nchini Syria kuwa ni kutwaa mji wa kale wa Palmyra wakati Marekani ikiwa imedhamiria kuendelea kushambulia ngome ya IS katika mji wa Raqqa.

Wanajeshi wa Syria katika moja ya oparesheni zake mjini RaqqaPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Kumekuwepo na mawasiliano ya karibu kati ya wapinzani hao ambao kila mmoja amekuwa akimshutumu mwenzake kuhusu  hali ya uhalibifu mjini Aleppo, Moscow inasema kuwa uhusiano huo hivi sasa umehifadhiwa katika hatua ya vitendo

Wakati hayo yakiendelea msemaji wa vikosi vya jeshi la Kikurd vinavyoungwa mkono na Marekani kaskazini mwa Syria amesema kuwa, wanakaribia kutwaa bwawa la kimkakati ambalo linadhibitiwa na kundi la IS kaskazini mwa nchi hiyo.

Msemaji huyo amesema kuwa katika siku za hivi karibuni wanajeshi wenye silaha wanaoungwa mkono na Marekani, pamoja na majeshi maalum ya Ufaransa na Uingereza wamefanikiwa kuwakomboa wanavijiji na kuchukua uthibiti wa mashamba, na kuongeza kuwa sasa wako karibu umbali wa kilometa 5 tu kufikia bwawa la Euphrates.

Wanajeshi wa jeshi la kidemokrasia la Syria ambalo ni muungano wa wapiganaji wa Kikurd na Kiarabu wamekuwa katika mashambulizi katika mji wa Raqqa tangu mwezi Novemba. Oparesheni ambayo inaungwa mkono na mashambulizi ya anga ambayo yanaongozwa na muungano wa Marekani yanalenga kutenga na kuuzirira mji wa Raqqa ambao ni ngome ya kundi la IS.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef