1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yapata waziri mkuu mpya

9 Agosti 2012

Rais Bashar al-Assad wa Syria amemteua waziri mkuu mpya kuchukua nafasi ya Riad Hijab aliyejitenga na utawala wake wiki hii. Na huko Iran unafanyika mkutano wa kujadili hali ya usalama nchini Syria.

Waziri mkuu mpya wa Syria, Wael al-Halki
Waziri mkuu mpya wa Syria, Wael al-HalkiPicha: Reuters

Mkutano kuhusu Syria ulifunguliwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Ali Akbar Salehi. Miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo ni wanadiplomasia kutoka nchi kama Urusi, Pakistan, Afghanistan na Iraq. Iran, ambayo ni mshirika wa karibu wa rais Bashar al-Assad, imeelezea nia yake ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Syria. Ingawa Iran imesema kwamba haitoruhusu utawala wa Assad uanguke, Salehi ameonyesha ya nia ya kuwaalika wapinzani wa Assad kufanya mazungumzo na serikali.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Ali Akbar SalehiPicha: Reuters

Waziri huyo alisisitiza pia kwamba ni lazima pafanyike mazungumzo kati ya waasi na serikali ili amani iweze kupatikana, na akaongezea kwamba mazungumzo ndio njia pekee ya kuumaliza mgogoro wa Syria. Kabla ya kuanza kwa mkutano wa leo, Iran ilionya kwamba hatua ya kumwondoa Assad madarakani kwa ghafla itakuwa na matokeo mabaya kabisa kwa Syria.

Waasi wajiondoa Salaheddin

Baada ya Riad Hijab, aliyekuwa waziri mkuu wa Syria, Jumatatu kutangaza kujitenga na serikali na kujiunga na wapinzani, Assad leo amemteua Wael al-Halqi kuchukua nafasi yake. Kabla ya hapo, Halqi alikuwa waziri wa afya wa Syria. Mwanasiasa huyo alisomea udakatari katika chuo kikuu cha Damascus. Kati ya mwaka 2000 na 2004, alikuwa katibu mkuu wa chama tawala katika mkoa wa Daraa. Mwaka 2010 alishikilia wadhifa wa uenyekiti wa chama cha madaktari.

Wakati mapigano baina ya wanajeshi wa Assad na waasi yakiendelea nchini Syria, jeshi huru la Syria limejiondoa kwenye wilaya ya Salaheddin ya mji wa Aleppo, ambayo kwa siku kadhaa ilikuwa ikipiganiwa na waasi na majeshi ya Assad. Akizungumza na shirika la habari la afp kwa njia ya simu, kamanda Hossam Abu Mohammed wa jeshi huru la Syria alithibitisha kwamba waasi wote wameondoka Salaheddin na kwamba wanajeshi wa serikali sasa wanaingia wilayani humo. Hata hivyo waasi wameeleza kwamba bado wanadhibiti zaidi ya asilimia 50 ya mji wa Aleppo.

Sehemu ya mji wa Aleppo iliyoharibiwa na vitaPicha: dapd

Wakati huo huo, rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, ameikasirisha serikali ya nchi yake iliyopo madarakani sasa, baada ya kusema kwamba hatua za haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa zinatakiwa kuchukuliwa ili kuumalizia mgogoro wa Syria. Sarkozy aliufananisha mgogoro wa Syria na ule wa Libya na kuashiria kwamba nguvu za kijeshi zinaweza kutumika kumwondoa Assad madarakani. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, alielezea kushangazwa kwake na kauli ya Sarkozy na kusema kwamba ni kauli ambayo haistahili kutolewa na mtu aliyewahi kuwa rais.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman