Syria yasisitiza mjadala wa kitaifa
21 Oktoba 2012Brahimi alikutana na waziri wa mambo ya kigeni Walid Muallem pamoja na viongozi wa upinzani wanaokubalika na rais Bashar al-Assad , katika juhudi za kupata kuungwa mkono mpango wake wa kupatikana usitishaji wa mapigano , wakati wa sikukuu muhimu ya Kiislamu wiki ijayo.
Lakini mazungumzo hayo yaligubikwa na hali ya wasi wasi katika nchi jirani ya Lebanon , ambako viongozi wa upinzani pamoja na waziri mkuu walihusisha shambulio lililosababisha mauaji ya afisa wa ngazi ya juu wa upelelezi na utawala wa Syria .
Nchini Syria kiasi watu 108 wameuwawa katika ghasia siku ya Jumamosi , 42 kati yao ni raia, limeripoti shirika la kuangalia haki za binadamu nchini humo, wakati mapigano yakiendelea katika maeneo ya kaskazini na kuzunguka mji wa Damascus.
Kusitisha mapigano
Wizara ya mambo ya kigeni imesema waziri Muallem amejadili pamoja na Brahimi, kile walichokiita "hatua ya kusitisha mapigano, ili kujitayarisha kwa mjadala wa dunia juu ya Syria, bila kuingiliwa na ushawishi wa mataifa ya nje".
"Mjadala wa aina hiyo ndio njia pekee ya kutoka katika mzozo huo", wizara hiyo imesema.
Muallem pia amelalamika kwa Brahimi juu ya mataifa ya eneo hilo ambayo Syria inayashutumu kwa kuwahifadhi, kuwapa silaha na kuwapa mafunzo waasi, akisema kuwa vitendo vyao vinaathiri ujumbe wa mjumbe huyo wa amani wa umoja wa mataifa ya mataifa ya Kiarabu, Arab League.
Uturuki na Saudia zalaumiwa
Syria imeilaumu mara kwa mara nchi jirani ya Uturuki pamoja na nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Saudi Arabia na Qatar kwa kuunga mkono wapiganaji waasi.
Brahimi ana matumaini ya kupata usitishaji wa mapigano wakati wa sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Adha, inayoanza Oktoba 26, akiamini kuwa hiyo inaweza kusafisha njia ya hatua za muda mrefu za amani.
Hassan Abdel Azim kutoka taasisi ya uratibu wa kitaifa kwa ajili ya mabadiliko ya kidemokrasia nchini Syria , kundi la upinzani linalovumiliwa na utawala wa nchi hiyo , ameunga mkono pendekezo hilo la kusitisha mapigano.
Usitishaji kama huo wa mapigano unaweza kusafisha njia kwa ajili ya hatua za kisiasa , iwapo utapanuliwa kujumuisha kuachiwa huru kwa wafungwa ambao wamekamatwa na utawala wa nchi hiyo pamoja na usambazaji wa msaada wa madawa kwa raia walioathirika, amesema. "Ghasia nchini Syria zimefikia katika kiwango cha kutisha ambacho kinatishia usalama na uhuru nchi hiyo", Abdel Azim ameongeza baada ya kukutana na Brahimi.
Nayo makundi ya upinzani
Ukichukua msimamo mkali zaidi , makundi ya upinzani ambayo yako nje ya nchi hiyo yanasema utawala wa Syria ni lazima uchukue hatua ya mwanzo na kusitisha mashambulio yake ya kila siku.
Brahimi anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Assad baadaye leo (21.10.2012) katika juhudi za ujumbe wake mjini Damascus kuleta amani.
Mjumbe huyo amefanya ziara katika mataifa kadha ambayo yana ushawishi katika mzozo huu wa Syria katika muda wa wiki moja iliyopita, ikiwa ni pamoja na ziara nchini Lebanon na Iran, na kuonya kuwa ghasia zinaweza kusambaa na kuliwasha moto katika eneo lote.
Mwandishi : Sekione Kitojo /afpe
Mhariri: Amina Abubakar