Syria yatakiwa kujenga upinzani imara
1 Novemba 2012Wachunguzi wa masuala nchini Syria pamoja na waasi,wanasema kuwa ongezeko la mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la serikali ni jaribio la utawala wa Rais Bashar al-Assad kugeuza mafanikio waliyoyapata waasi.
Ndege za kivita zimeshambulia katika maeneo ya vitongoji vya mji unaoshikiliwa na waasi wa Harasta, mashariki ya mji mkuu Damascus, wakati helikopta za kijeshi zilishambulia wilaya moja ya mji huo mkuu leo.
Kwa mujibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria , jeshi la anga pia limeshambulia miji katika jimbo la kaskazini magharibi la Idlib, ambalo sehemu kubwa ya jimbo hilo inadhibitiwa na waasi.
Ghasia hizo zimekuja siku moja baada ya watu karibu 152 kuuwawa nchini Syria, 58 wakiwa ni raia, 48 ni waasi na wanajeshi wa serikali 46, limesema shirika hilo la haki za binadamu.
Mashambulizi ya anga , wamesema wadadisi wa mambo kuwa hayaelekezwi zaidi dhidi ya waasi lakini yanasababisha hofu kubwa miongoni mwa raia na kuchochea hasira kwa raia wa kawaida ili kupambana na wapiganaji waasi waliomo miongoni mwao.
Mafanikio ya wapiganaji
Wapiganaji wamepata mafanikio kadha katika wiki chache zilizopita, hususan upande wa kaskazini, na jeshi la anga la Syria linaona hali hii kuwa ni kitisho, amesema Charles Lister, mchambuzi mwenye makao yake makuu mjini London anayefanyakazi na kituo cha IHS Jane, kinachohusika na masuala ya uchunguzi wa ugaidi na mapambano ya wapiganaji.
Clinton aonya
Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton , akitoa ishara ya kuchukuliwa hatua imara zaidi na serikali ya Marekani katika juhudi za kuunda upinzani wa kisiasa wenye kuaminika dhidi ya rais wa Syria Bashar al-Assad, amesema kuwa mkutano utakaofanyika wiki ijayo nchini Qatar utakuwa nafasi ya kupanua muungano wa wapinzani dhidi ya Assad.
"Huu hauwezi kuwa upinzani unaowakilishwa na watu ambao wana malengo mengi tu mazuri , lakini kwa wakati mwingi hawajakuwa ndani ya Syria kwa zaidi ya miaka 20,30, au 40," amesema Clinton wakati wa ziara yake nchini Croatia.
Clinton pia ameonya kuwa Marekani inahitaji kuusaidia upinzani nchini Syria kuungana na kupambana na utawala wa rais Bashar al-Assad, lakini ameutaka upinzani kujitenga na juhudi za wale wenye msimamo mkali ambao wanataka kuteka mapinduzi ya nchi hiyo.
Matamshi ya Clinton yanawakilisha mtazamo wa kuachana na baraza la taifa la Syria, SNC, ambalo ni kundi lililopo nje ya nchi, kundi ambalo limekuwa likitoa matamshi ya kupinga kuingilia kati kwa jumuiya ya kimataifa katika mzozo nchini Syria.
Maafisa wa Marekani wamekuwa wakieleza pembeni kutoridhishwa kwao na uwezo wa baraza hilo la taifa la Syria , kuja pamoja na mpango wenye kueleweka na kushindwa kwao kuyaunganisha makundi ya ndani ya Syria ambayo yamekuwa yakipambana kwa muda wa miezi 19 sasa dhidi ya utawala wa Assad.
Wanachama waandamizi wa baraza la taifa la Syria, jeshi la ukombozi wa Syria FSA na makundi mengine ya waasi yamemaliza mkutano wao nchini Uturuki jana na kupendekeza muungano wa serikali ya mpito katika miezi ijayo.
"Ni mgawanyiko uliopo kwetu ambao umeruhusu majeshi ya Assad kufikia hadi hapa tulipo", Amesema Ammar al-Wawi , kamanda wa jeshi la waasi , ameliambia shirika la habari la reutres baada ya mazungumzo nje kidogo ya mji mkuu Istanbul.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef