1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSyria

Syria yatangaza kusitisha mapigano na wanamgambo wa Kikurdi

Dotto Bulendu
9 Januari 2026

Wizara ya ulinzi ya Syria imetangaza hatua ya kusitisha mapigano katika mji wa Aleppo baada ya mapigano makali ya siku kadhaa kati ya jeshi na wapiganaji wa Kikurdi yaliyowalazimisha maelfu ya raia kuukimbia mji huo.

Syria Aleppo 2026 | Wanajeshi wa serikali baada ya mapigano na wapiganaji wa Kikurdi
Wanajeshi wa serikali ya Syria wakiwa wameketi kwenye meli yao ya kubebea silaha (APC) kufuatia mapigano na wapiganaji wa Kikurdi katika eneo linalogombaniwa la mji wa kaskazini wa Aleppo, Syria, Jumatano, Januari 7, 2026.Picha: Ghaith Alsayed/AP Photo/picture alliance

Watu 21 wameuawa katika ghasia hizo. Wizara hiyo ya Ulinzi imetangaza hatua ya kusitisha mapigano karibu na vitongoji vya Sheikh Maqsud, Ashrafiyeh na Bani Zeid katika jiji la Aleppo.

Marekani kupitia ukurasa wa X wa mjumbe wake Tom Barrack imeunga mkono uamuzi huo wa kusitisha mapigano na kusema inatumai kufanyika kwa mazungumzo ya utulivu na ya kina ili kuongeza wigo wa usitishaji mapigano na kuleta maelewano kati ya pande zinazopigana ingawa Makundi ya Kikurdi yanapinga kujiondoa kutoka Aleppo.

Syria imekuwa ikipambana na vikosi vya SDF mjini Aleppo

Tangu Jumanne, vikosi vya serikali ya Syria vimekuwa vikipigana na Kikosi cha SDF cha Wakurdi kinachoungwa mkono na Marekani huko Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria.

Wapiganaji wa Kikurdi walipewa hadi saa 3:00 asubuhi ya ijumaa kuwa wameondoka katika maeneo waliyokuwa wameweka kambi, uamuzi huo umepokelewa kwa furaha na baadhi ya raia wa mjini Aleppo 

Raia wakiwa wamebeba mizigo na mali zao wanapokimbia kufuatia mapigano mapya kati ya jeshi la Syria na Vikosi vya SDF, huko Aleppo, Syria, Januari 8, 2026.Picha: Mahmoud Hassano/REUTERS

Zakaria al-Mohammed amesema "Tumekuwa katika vita kwa miaka takriban  14,inatosha sasa, tunataka kuishi kwa amani na tunataka amani, hakuna zaidi.Tunazihimiza nchi za kigeni kuwashinikiza wanamgambo wa SDF waondoke Syria.”

Ghasia hizo ni changamoto ya hivi punde kwa Syria ambayo bado inajitahidi kupata mustakabali mpya baada ya utawala wa muda mrefu wa Bashar al Assad kuondolewa madarakani zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Israel na Uturuki zimekuwa zikigombea ushawishi nchini Syria

Uturuki, ambayo inapakana na Syria  ilifanya mashambulizi mfululizo kuvisukuma vikosi vya Wakurdi kutoka mpakani. Israel na Uturuki zimekuwa zikigombea ushawishi nchini Syria tangu kupinduliwa kwa Assad mwezi Disemba 2024.

Askari wa serikali ya Syria akimsaidia mwanamke mzee anayekimbia kutoka vitongoji vya Sheikh Maqsoud na Achrafieh baada ya mapigano kuzuka Jumanne kati ya vikosi vya serikali ya Syria na wapiganaji wa Kikurdi katika eneo linalogombaniwa la mji wa kaskazini wa Aleppo, Syria, Jumatano, Januari 7, 2026.Picha: Omar Albam/AP Photo/picture alliance

Wakati huohuo Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa amekutana na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen siku ya Ijumaa, vyombo vya habari vya serikali vimesema, Von der Leyen ni afisa wa juu zaidi wa Umoja wa Ulaya kuitembelea Syria tangu Bashar al-Assad aondolewe madarakani na vikosi vya Sharaa mnamo Desemba mwaka 2024. Umoja wa Ulaya imeahidi karibu euro bilioni 2.5 kwa Syria kwa kipindi cha mwaka 2025 na 2026.

Von der Leyen anafanya ziara ya kikanda pamoja na rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa.Taarifa ya pamoja ya Umoja wa Ulaya na Jordan iliyotolewa kabla ya viongozi hao kuwasili mjini Damascus imesema Umoja wa Ulaya na Jordan zitaendelea kuunga mkono utawala jumuifu wa Syria chini ya wasyria wenyewe.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW