1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yatishia kujibu mashambulizi ya Israel

10 Mei 2013

Syria imetishia kujibu mashambulio yoyote mapya kutoka Israel huku washirika wake wanamgambo wa Hezbolla wakisema Syria itawapa silaha zitakazobadili kile walichokitaja kuwa silaha za kubadilisha hali ya mambo.

Mzozo wa Syria na Israel
Mzozo wa Syria na IsraelPicha: MENAHEM KAHANA/AFP/Getty Images

Naibu waziri wa mambo ya nje Faisal Muqdad amesema maagizo yametolewa ya kukabiliana mara moja na shambulio lolote jipya kutoka Israel.

Duru kadhaa za Israel zimesema mashambulio ya Ijumma na Jumapili wiki iliyopita yalilenga shehena ya silaha zilizokuwa zikipelekwa kwa kundi la Hezbollah la nchini Lebanon lakini Muqdad amekanusha madai hayo.

Kerry na Lavrov wazungumzia SyriaPicha: Reuters

Syria imeukaribisha mpango wa pamoja wa Marekani na Urusi wa kutafuta suluhisho la kisiasa ili kumaliza vita vya miaka miwili lakini wakati huo huo imeshutumu sharti la Marekani la kumtaka Rais Bashar al Assad kujiuzulu.

Assad yuko tayari kwa wachunguzi

Serikali ya rais Assad imesema pia iko tayari kupokea kundi la Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya kutumika kwa silaha za kemikali nchini humo.

Na mjini Beirut,kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah amesema Syria italipa kundi lake silaha alizozitaja kuwa zitakazobadili mkondo wa mambo yalivyo sasa na kukabiliana na Israel kutoka eneo la milima la Golan.

Israel ilinyakua eneo hilo la Golan kutoka kwa Syria katika vita vilivyodumu kwa siku sita mwaka 1967. Israel imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa itaingilia kati kuzuia kupewa kwa wanamgambo wa Hezbollah silaha.

Hezbollah inashirikiana na majeshi ya Assad katika maeneo kadhaa nchini Syria.Utawala wa Assad unategemea pakubwa usaidizi wa wanamgambo hao na gazeti moja la Lebanon Al Akhbar limemnukuu Assad akisema kuwa Syria italipa kundi hilo chochote kwa uaminifu wake.

Kiongozi wa Hezbollah Hassan NasrallahPicha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Huku hayo yakijiri,waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino Albert del Rosario amesema kuwa amependekeza kwa Rais Benigno Aquino III kuwaondoa wanajeshi wake wa kulinda amani katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kutoka eneo la Golan kufuatia kutekwa nyara kwa wanajeshi wake wanne na waasi wa Syria.

Hiki ni kisa cha pili cha utekaji nyara katika kipindi cha miezi miwili na del Rosario amesema serikali inaamini kuwa hatari inayowakabili wanajeshi wake 342 imepita viwango vya kuvumilika.

Wanajeshi wa Ufilipino watekwa nyara

Waasi waliwateka nyara wanajeshi hao katika mpaka unaotenganisha Syria na Israel siku ya Jumanne, miezi miwili baada ya wanajeshi wengine 21 wa kulinda amani kutoka Ufilipino kutekwa nyara na kuzuiliwa kwa siku tatu katika eneo hilo hilo.

Umoja wa Mataifa umesema mjumbe wake maalum kuhusu Syria Lakhdar Brahimi ameacha mpango wake wa awali wa kujiuzulu na kwamba atasalia kuhudumu baada ya makubaliano ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Syria ulioafikiwa kati ya Urusi na Marekani.

Katika taarifa nyingine, Isreal imeiarifu Marekani kuwa Urusi ina mipango ya kuiuzia Syria silaha zinazoweza kufanya mashambulio kutoka ardhini hadi angani.Urusi imeendelea kuiuzia Syria silaha katika kipindi chote cha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimewauwa watu takribani 70,000.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Ap
Mhariri:Daniel Gakuba.