1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili wametakiwa kufuatilia misaada yao inavyotumika

28 Juni 2019

Shirika la Utetezi wa Haki za Binadamu Duniani la Human Rights Watch, limesema serikali ya Syria inaitumia misaada ya kiutu inayopokea kuwaadhibu wapinzani na vile vile kuwafaidisha wanaoiunga mkono.

Syrische Flüchtlinge in Ägypten El Obour
Picha: picture-alliance/dpa/P. Rigol

Ripoti iliyotolewa hii leo na shirika hilo la haki za binadamu ulimwenguni imeeleza kwamba shirika moja linalofanyakazi kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa lilishirikiana na  kikundi kimoja kilichoundwa na mwanachama mmoja wa jeshi la ulinzi la taifa la Syria kufanya mradi lakini baada ya miezi sita shirika hilo liligundua mradi huo haukutekelezwa licha ya kupokea fedha kutoka kwa Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo pia bila kutaja majina ya wakuu serikalini inaeleza kwamba viongozi hao walio na hisa kubwa katika biashara mbali mbali wamekuwa wakifadhili makundi yanayoiunga mkono serikali ya Syria, hivyo basi kuwataka wafadhili na wawekezaji kuhakikisha michango yao inatumika vyema kwa ajili ya watu wa Syria. Aidha imewatahadharisha wawekezaji na wafadhili kwamba wanaweza kuhusishwa katika kufadhili makundi ya wahuni pasi na wao kujua.

Kaimu mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati, Lama Fakih, amesema sheria  waliyoiunda Syria inahujumu haki za biandamu kwa hivyo wafadhili wanafaa kuhakikisha hawashirikiani na serikali katika kukiuka haki za biandamu.

Kaimu mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati, Lama FakihPicha: privat

Syria inahitaji miaka 15 kujengwa upya

Ripoti hiyo ambayo imewahoji watu 33 wakiwemo wafanyakazi wa utoaji misaada, wafadhali, wataalmu na walengwa wa misaada hiyo pia imeeleza kwamba fedha zínazotumiwa kwa miradi ya ujenzi na urekebishaji wa miundombinu zinaweza kusaidia makundi mbali mbali kuendelea kuwafurusha watu kwa lazima kutoka katika makao yao, kuwatesa na kukamatwa.

Tangu kuanza kwa vita nchini Syria mwaka 2011, taifa hilo limeporomoka, sehemu kubwa ya nchi hiyo imeharibiwa kabisa na Syria inalenga kuijenga upya nchi  hiyo kwa muda wa miaka 15. Wanakisia gharama za kufanya hivyo ni dola bilioni 200. Jamii ya kimataifa imeombwa kusaida katika hilo sawa na kuwasaida Wasyria zaidi ya milioni 11 wanaohitaji msaada baada ya kuyakimbia makaazi yao kwa vita. Mwezi Machi mwaka huu katika kongamano la kuichangia kifedha Syria, wajumbe waliweka ahadi ya kutoa kiasi cha dola bilioni saba. Kwa sasa wananchi nchini humo wanaishi kwa kutegemea misaada ya kiutu huku wakizongwa na ufukara na ukosefu wa chakula na dawa.

Lama Faki ameeleza katika ripoti hiyo ya kurasa 91 kwamba jitihada zisipofanywa za kubadilisha mifumo inayotumika na mashirika ya kiutu na wawekezaji basi wako katika hatari ya kufadhili vyombo vya ukandamizaji vya serikali ya Syria. 

(APED/PAE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW