1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syriza yashindwa lakini Ugiriki bado i mashakani

18 Juni 2012

Vyama vinavyopendelea Ugiriki kusalia kwenye Kanda ya Euro vimefanikiwa kupata wingi wa kutosha bungeni kuunda serikali na kukitenga chama cha mrengo mkali (SYRIZA) ambacho kilishaapa kuitoa nchi hiyo kwenye Euro.

Kiongozi wa chama cha New Democracy cha Ugiriki, Antonis Samaras.
Kiongozi wa chama cha New Democracy cha Ugiriki, Antonis Samaras.Picha: Reuters

Ilikuwa ni siku refu iliyomalizika kwa aina fulani ya kuvuta pumzi kwa Ugiriki na Ulaya. Baada ya uchaguzi wa bunge wa hapo jana, sasa bunge la Athens linaongozwa na vyama ambavyo vinaunda mkono Ugiriki kubakia kwenye kanda ya sarafu ya euro na kuendelea kwa mpango wa kubana matumizi na mageuzi ya kiuchumi.

Mshindi wa wazi chama cha kihafidhina cha New Democracy (ND) kinachoongozwa na na Antonis Samaras, kina uwezekano mkubwa wa kuunda serikali ya mseto na wasoshalisti wa PASOk cha Evangelos Venizelos. Vyama viwili ambavyo ndivyo vilivyohusika kuibomoa nchi kwa sera zake, sasa vinalazimika kuiinua.

Ni wazi kuwa kazi hii haitakuwa rahisi. Kwa sasa Ugiriki inaishi kwa msaada wa kifedha kutoka wakopeshaji wa kimataifa, Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Umoja wa Ulaya na Benki ya Umoja wa Ulaya. Vyama vya ND na PASOK vimewaahidi wapiga kura makubaliano mapya kwa kanuni zinazohusika na mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya.

Kazi ngumu huko mbele

Lakini fursa ya majadiliano na makubaliano mapya ni finyu sana. Na si kwa sababu wakopeshaji hawataki makubaliano, ambazo ndizo shaka zilizoenea sana nchini Ugiriki, lakini kwa kuwa washirika hao wana wasiwasi na siasa za Kigiriki.

Spiros Moskovou wa Idhaa ya DW Kigiriki, mwandishi wa tahriri hii.Picha: DW

Kwa mfano, kwa miaka mitatu iliyopita serikali imeshikilia kukata idadi ya wafanyakazi na mafao ya uzeeni kama hatua za mageuzi ya kiuchumi, lakini imekuwa ikifanya machache kuwabana wakwepa kodi. Sasa ghafla hii moja, ND na PASOK wanataka kuyafanya mambo kuwa bora zaidi, suali ni ikiwa watawezaje?

Serikali mpya ya Ugiriki itapata tabu sana katika kuweka mizani sawa. Baada ya nenda-uje zote za miaka michache iliyopita, sasa ukuwaji wa uchumi lazima uwe mkubwa na wa haraka mno kuweza kuwaridhisha washirika wa kimaendeleo.

Na wakati huo huo inakabiliwa na umma usio na uhakika wa maisha yake, ambao ulishitushwa na kutikisika sana kwa mporomoko wa uchumi. Serikali hii inalazimika kuidhinisha hatua mpya – na pengine kali zaidi – ikiwa kweli inataka kubadilisha hali.

Jambo la kutia moyo ni kwamba nje ya mipaka ya mataifa ya kusini ya Umoja wa Ulaya, kuna waungaji mkono kama Ujerumani na Ufaransa, ambao hawako tayari kuiona nchi moja ya Ulaya ikienda. Hata hivyo, mataifa hayo nayo hayataki mwanachama yeyote abakie bila kutekeleza kwa ukamilifu mpango wa kuinua uchumi wake. Na Ugiriki haiwezi kuwa tafauti kwa kila hali.

Ndani ya Ugiriki kwenyewe, uchaguzi huu si kwamba umetoa ushindi kwa ND na PASOK tu, bali pia chama kilichochukuwa nafasi ya pili cha SYRIZA, kinachoongozwa na mwanasiasa kijana mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kushoto, Alexis Tsipras.

Kijana huyu, hata kama kwa wakosoaji wake ameshindwa kuwa mwanasiasa mwenye mawazo ya ujenzi, bado hakuna shaka kuwa amekuwa na mvuto mkubwa. Ameweza kukipatia chama chake kidogo na kipya jumla ya asilimia 27 ya kura zote. Alitaka kuuchana mkataba wa mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya na Ugiriki.

Na hata kama sasa Ulaya itavuta upumzi wa kupumua kwa sababu SYRIZA haikufanikiwa kuibuka kama chama pekee chenye nguvu nchini Ugiriki, lakini chama hicho hakitachelea kuonesha uwezo wake mbele ya serikali, bungeni na mitaani. Juu ya yote, mtu hawezi kufikiria kuwa eti serikali mpya ya Ugiriki iko kwenye furaha. Jukumu lililoko mbele yake ni kubwa mno kuweza kuipa muda wa kufurahia.

Mwandishi: Spiros Moskovou/DW Kigiriki
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW