Taarifa za michezo katika juma
4 Septemba 2015Wanariadha wa Kenya walioshiriki katika mashindano ya ubingwa wa dunia yaliokuwa yakifanyika mjini Bejing na kumalizika Jumapili iliopita, walirejea nyumbani hiki na kupokewa kwa shangwe baada ya ushindi wao mkubwa ambapo Kenya ilimaliza nafasi ya kwanza katika orodha ya medali na kuwaangusha miamba kama Jamaica na Marekani. Maelfu ya watu pamoja na viongozi wa taifa hilo la Afrika mashariki walimiminika kuwalaki wanariadha hao katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenyatta mjini Nairobi. Kenya ilinyakua medali saba za dhahabu, sita za fedha na tatu za shaba na kushika nafasi ya kwanza kwa mara ya kwanza tangu michezo hiyo ya riadha ya ubingwa wa dunia ilipoanza mwaka 1983. Halikadhalika kulitawazwa mabingwa wawili wasio tarajiwa nao ni Julius Yego katika urushaji mkuki kwa wanaume na Nicholas Bett aliyeshinda mbio za mita 400. Makamu wa rais William Ruto alisema mashujaa wa Kenya wameushtuwa ulimwengu akiongeza Kenya sio nchi kubwa duniani wala yenye nguvu lakini ni nchi ilio bora, kabla ya kuwakaribisha chai wanariadha hao kwa nyumbani kwake.Waziri wa michezo Hassan Wario alisema mafanikio ya kikosi cha riadha cha Kenya yanatoa matumaini kwa michezo ya Olimpiki mwaka ujao huko Rio de Janeiro Brazil, lakini akaongeza bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kuhakikisha inakuwa na uwakilishi bora. Jee baada ya mafanikio hayo,kuna mipango yoyote ya kuimarisha riadha hadi maeneo ya mashambani
Wakati huo huo, Makamu wa rais wa Kenya William Ruto, alitangaza mipango ya kuwachukulia hatua watakaohusika na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu baada ya wanariadha wawili wa Kenya kugunduliwa kutumia madawa hayo wakati wa mashindano ya Beijing. Ruto alisema suala hilo litajadiliwa katika baraza la mawaziri. Akaongeza n kwamba wanataka kuupa nguvu wakala wa kupambana na madawa hayo nchini Kenya na kuupa utaratibu wa kisheria kukabiliana na kosa la aina hiyo.
Afrika Kusini imeahidi kwamba itafanya maandalizi kabambe wakati jiji lake la Durban litakapoandaa michezo ya Jumuiya ya madola-commonwealth 2022, na kwamba michezo hiyo itasaidia kuibadili sura ya enezi ya misukosuko iliolikumba taifa hilo miaka iliopita.Afrika kusini iliwahi kuandaa mashindano ya kombe la dunia la mchezo wa Rugby 1995 na lile la dunia la kandanda 2010 , ambayo yalikuwa ya mafanikio makubwa katika juhudi zake za kushajiisha umoja wa kitaifa baada ya kumalizika enzi ya sera ya ubaguzi wa rangi-Apartheid .
Mamia walimiminika kusikia kutoka New Zealand tangazo la mji huo wa Durban kupewa nafasi ya kuandaa mashindano ya Jumuiya ya madola 2022 huku ukishangiria, na itakuwa ni mara ya kwanza yanafanyika barani Afrika. Mji wa Edmonton Canada ulijitoa katika kinyanganyiro cha kuwania kuwa mwenyeji wa mashindano ya 2022 pakitajwa miongoni mwa sababu nyengine kuwa ni pamoja na matatizo ya fedha yanayohusiana na bei ya mafuta, na hivyo kuiacha Afrika Kusini kuwa mgombea pekee.
Kandanda:
Mchezaji wa Kimataifa wa Ujerumani Kevin Grosskreutz anahamia Galatasaray ya Uturuki kutoka kilabu ya Bundesliga ya Borussia Dortmund , ingawa hatua hiyo ilikuwa haijakamilika muda wa mwisho wa usajili majira ya joto ulipofika. Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA limesema usajili wake hakuweza kushughulikiwa mapema na kusajiliwa kwake hakuwezi kuotrodheshwa sasa hadi Januari mosi. Hata hivyo Gosskreutz mwenye umri wa miaka 27 alikuwemo katika kikosi cha Ujerumani kilicholinyakua kombe la dunia 2014 ataondpoka Dortmund na kujiunga na mchezaji mwengine wa Ujerumani Lukas Podolski katika kilabu ya Galatasaray, akiruhusiwa kufanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki hadi suala lake la usajili litakapopata kibali cha FIFA.
Vilabu vya kigeni ndivyo vinavyonufaika zaidi kutokana na vitita vya usajili na malipo ya kuhama wachezaji panapohusika na ligi kuu ya kandanda ya England Premier League. Wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema hali hiyo itaendelea kuwa hivyo, kwasababu ya kuongezeka kwa mapato ya matangazo ya mpira. Usajili unakamilika wiki hii. Ingawa malipo mengi ya vitita vya fedha hayatangazwi bayana, kwa jumla inakubaliwa kwamba katika mikataba 10 ya vitita vya vikubwa inayohusiana na vilabu vya ligi vya England, saba ni ya wachezaji waliosajiliwa kutoka ligi nyengine.
Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga imenufaika zaidi, huku Wolfsburg, Hoffenheim na Bayer Leverkusen zikijipatia karibu pauni 100 milioni sawa na dola 153 milioni za Kimarekani kati yao, kwa ajili ya Kevin de Bruyne alisajiliwa na Manchester City kutoka Wolfsburg, Hoffenheim imemuuza Robert Firmino kwa Liverpool na Son Heung-min anahamia Tottenham hotspur kutoka Bayer Levekusen. Malipo jumla kwa vilabu vya nje ya pauni 585 milioni yalikuwa ni asilimia 10 zaidi ya matumizi ya mwaka uliopita , wakati mwaka 2012 yalikuwa pauni 300 milioni .
Mgombea urais wa Shirikisho la kandanda la kimataifa FIFA Mkorea Chung Mong-Joon amelishitumu Shirikisho la kandanda barani Asia kwa kuendesha vitendo vya hila ili kuumuunga mkono mpinzani wake Michael platibni. Chungu amesema Shirikisho hilo AFC ambalo rais wake Sheikh Salman bin Ibrahim al Khalifa amemuunga mkono hadharini Platini, limetuma barua karibu kwa kila chama mwanachama wa Shirikisho hilo la soka la Asia isipokuwa tu Korea Kusini na Jordan, ili kumpigia debe Platini. Mwanamfalme Ali bin Hussein wa Jordan pia yumo kwenye kinyanganyiro hicho cha kuwania Urais wa FIFA kufuatia kujiuzulu kwa Sepp Blatter . Platini anapewa nafasi kubwa ya kushinda akiwa anaungwa mkono na vyama muhimu vya kitaifa vya kandanda na mashirika ya mchezo huo ya kanda. Lakini Chung anasema Platini asingefaa kuwa mgombea kwa sababu alikuwa nan uhusiano wa karibu na Blatter. Uchaguzi wa kumpata rais mpya wa FIFA utafanyika Februari 26 mwakani.
Mshambuliaji wa Bulgaria Dimitar Berbatov amejisajili na PAOK ya Ugiriki kwa msimu mmoja. Hayo yametangazwa na kilabu hiyo ya ligi kuu ya Ugiriki ambayo haikutoa maelezo zaidi kuhusu usajili huo, lakini vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kwamba Berbatov mwenye umri wa miaka 34 na mchezaji wa zamani wa Manchester united atalipwa kitita cha euro milioni mbili kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja na kilabu hiyo. Mchezaji huyo alikuwa awali asajiliwe na kilabu ya England ya aston villa, lakini makubaliano yakavunjika wiki hii. Pia aliwahi kuzichezea Tottnham Hotspur ya Uingereza, bayer Leverkusen ya Ujerumani na CSKA ya Sofia Bulgaria. Berbatov aliichezea timu ya taifa ya Bulgaria kuanzia 1999 hadi 201 akishiriki mechi 78 na kufunga mabao 48.
Chile, mabingwa wa kombe la Amerika-Copa America- imepanda nafasi mbili juu hadi nafasi ya 8 katika orodha ya timu bora ya Shirikisho la kandanda la kimataifda FIFA, huku Arngetzina ikiongoza. Chile imechukua nafasi ya England ambayo imeshuka hadi nafasi ya 10. Ubeligiji imeipiku Ujerumani ikishika nafasi yake ya pili na kuiacha ikiwa ya tatu, Colombia iko nafasi ya nne na Brazil ya tano. Kwa upande wa nchi za kiafrika, inayoongoza ni Algeria ikishika nafasi ya 19 katika orodha ya dunia. Kwa upande wa mataifa ya Amerika kati na eneo la Caribbean Mexico inaongoza kanda hiyo ikiwa nafasi ya 26 katika orodha jumla ya timu bora duniani wakati Iran ikiongoza kwa upande wa Asia ikiwa nafasi ya 40.
Ubondia:
Bondia Floyd Mayweather Jr anajiandaa kusalia bondia asiyeshindwa akijiita bondia bora wa wakati wote, wakati atakapopambana na Mmarekani mwenzake mjini Las Vegas wiki ijayo. Mayweather atakuwa analitetea taji lake la dunia uzito wa Welter na ikiwa atashinda atasawazisha rekodi ya kutoshindwa katika mapigano 49 ya bingwa wa zamani wa uzto wa juu Rocky Maciano. Hata hivyo anasema hatotaka kuingia tena ringini kwa mara ya 50. Mayweather mwenye umri wa miaka 38, amesema na hapa ninamnukuu-“ Pambano la 49 litakuwa la mwisho, afya yangu ni muhimu zaidi. Lolote linaweza kutokea katika ndondi. Sihofii kushindwa.Unaweza kupata fedha nyingi lakini pia inawezekana ukashindwa kuzungumza tena, kutembea au kuwa na fahamu. Hivyo baada ya pambano hilo la 49 nitasema kwaheri .
Wengi lakini wana shaka shaka kama kweli bondia huyo atastaafu baada ya pambano hilo la Septemba 12, wakihoji kwamba Mayweather alisema hivyo hivyo hapo kabla lakini miezi 21 baadae akarudi ringini tena kupigana na Juan Manuel Marquez wa Mexico Septemba 2009 .