Taasisi ya kupambana na rushwa Kenya yaimulika KEMSA
25 Septemba 2020Taarifa hiyo imeelezwa katika ripoti iliyowasilishwa katika bunge la seneti. Kamati ya maadili na kupambana na rushwa ilianza kuchunguza tuhuma za ubadhirifu katika manunuzi ya vifaa vya dharura vya kupambana na corona vilivyokuwa vikitolewa na mamlaka ya usambazaji wa vifaa vya matibabu nchini humo.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, kulikuwa na "matumizi yasiyo ya kawaida,” ya shilingi za Kenya bilioni 7.8 sawa na dola za Kimarekani milioni 71.96.
Haya yamewekwa hadharani wakati watoa huduma za afya katika taifa hilo la Afrika ya mashariki wakiwa tayari wameshafanya migomo kadhaa kwa madai kuwa wanapatiwa malipo duni na kwamba wanatumia mavazi ya kujikinga na COVID 19 yasiyo na ubora wakati wa kuwatibu wagonjwa wenye maambukizi ya corona.
Soma pia: Kagwe: Hakuna fedha ya COVID-19 iliyotafunwa Kenya
"Uchunguzi ulionyesha kuwa kulikuwa na makosa ya kihalifu kwa upande wa maafisa wa umma katika manunuzi na ugawaji wa bidhaa za dharura za kupambana na COVID-19 Kwenye mamlaka ya usambazaji wa vifaa vya matibabu (KEMSA) hali iliyosababisha matumizi yasiyo ya kawaida ya fedha za umma.” Imesema sehemu ya ripoti ya kamati hiyo.
Kamati yapendekeza waliohusika na ubadhirifu wafunguliwe mashtaka
Kamati hiyo iliwasilisha taarifa hiyo ya uchunguzi wake wa awali kwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma na imependekeza mashtaka dhidi ya badhi ya maafisa, pamoja na kuangaliwa upya kwa mfumo wa manunuzi wa mamlaka husika ili "kuziba mianya ya ufisadi katika siku zijazo.”
Hata hivyo msemaji wa wizara ya afya hakupatikana kuzungumzia taarifa ya uchunguzi huo. KEMSA ni taasisi ya serikali iliyo chini ya wizara hiyo. Mkuu wa taasisi hiyo alisimamishwa kazi mwezi uliopita kutokana na tuhuma kuwa mamlaka hiyo ilizalisha vifaa vyenye ubora wa chini ya kiwango na kupandisha bei ya vifaa vingine.
Soma pia: Majaribio ya chanjo ya COVID-19 yaidhinishwa Kenya
Katika taarifa nyingine Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi iliorodhesha matukio ya bei na bidhaa zilizodaiwa kupandishwa bei na mamlaka hiyo ya usambazaji wa vifaa vya matibabu.
Vidonge vya Paracetamol vilivyokuwa vikiuzwa kwa Shilingi 40 za Kenya kwenye pakiti moja, viliuzwa kwa shilingi 66.50 wakati wa janga la corona wakati vitakasa mikono vilivyokuwa vikiuzwa shilingi 313 hapo awali, vilinunuliwa kwa shillingi 495.
"Hakuna Ushahidi unaoonyesha kuwa bei zilizoonyeshwa zilipatikana kwa kufuata utafiti wa masoko.” Imeeleza ripoti hiyo.
Chanzo: rttr