1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katika siasa za Ujerumani, wanawake bado wana safari ndefu

12 Novemba 2018

Wanawake wana uwakilishi usio sawa katika siasa za Ujerumani licha ya Kansela Angela Merkel kuwapo madarakani. Ndivyo inavyosema tathmini ya miaka 100 tangu wanawake walipopata haki ya kupiga kura katika taifa hilo.

100 Jahre Frauenwahlrecht
Picha: picture-alliance/M. Schreiber

Wanawake wanachangia zaidi ya nusu y wapigakura nchini Ujerumani, lakini uwakilishi wao bungeni hauwiani na wingi wao - chini ya theluthi moja ya wabunge ndiyo wanawake, uchache wa namna hii ulishuhudiw amara ya mwisho mwaka 1998. Hali ni mbaya zaidi hata katika mabunge ya majimbo ya shirikisho na manispaa za miji.

Ofisi ya heshima kwa wanaume

"Siasa nchini Ujerumani zinahodhiwa na wanaume, hilo likianzia kwenye siasa za miji na manispaa," anasema mtalaamu wa masuala ya siasa Helga Lukoschat, mkuu wa shirika la EAF, linalopigania fursa sawa. Mara nyingi maisha ya kisiasa huanzia katika mabaraza serikali za miji. Lakini wanaojihusisha kwa ngazi ya mashinani wanafanya hivyo kwa njia ya kujitolea na wanalaazimika kutenga muda kwa ajili ya mikutano.

"Ni vigumu kwa wanawake wanaoendelea kubakia nyumbani na kuangalia watoto,"  anasema Lukaschat. Hivyo haishangazi kusikia kwamba ni moja tu ya mameya kumi nchini Ujerumani ndiye mwanamke.

Wanawake wakiandamana mjini Berlin, Mei 12 1912 kudai haki ya kupiga kura.Picha: picture-alliance/akg-images

"Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu," anasema Ina Scharrenbach, mwenyekiti wa tawi la wanawake wa chama cha CDU katika jimbo la North-Rhine Westphalia na waziri wa usawa jimboni humo. Kunapaswa kuwa na kiongozi anaesema 'tunataka hilo'. Helga Lukoschat anakubaliana kwamba kuna idadi kubwa ya wanawake wene uwezo. "Vyama vinapaswa kuwaangazia hasa wanawake, kuunda mitandao ya ndani na kushughulikia zaidi mahitaji yao, kwa mfano kuahirisha nyakati za mikutano.

Kipengele cha nguvu ya sheria ya uchaguzi

Sheria ya uchaguzi ya ujerumani pia ni kikwazo kwa wanawake. Nchini Ujerumani mtu anaweza tu kuingia bungeni ama kwa kuchaguliwa moja kwa moja au kupata nafasi kwenye orodha. Katika uchaguzi wa bunge mwaka 2017, moja tu kati ya wabunge wa  kuchaguliwa moja kwa moja ndiyo alikuwa mwanamke. "Mara nyingi wanaume wanaogombea na kufanikiwa hawaachi kujaribu tena," anasema Helga Lukoschat. Kuna hali inayoendelea bado kwamba wapigakura wengi wanamwamini zaidi mwanaume.

Uwiano mdogo wa wanawake katika bunge la sasa la Ujerumani Bundestag unaweza pia kuelezewa na uingiaji wa vyama viwili vinavyodhibitiwa na wanaume: Chama cha AfD na kile kinachoegemea biashara cha FDP, kilichorejea katika Bundestag baada ya kuwa nje kwa miaka minne. Katika chama cha FDP, uwiano wa wanawake ni asilimia 23, katika AfD ni chini ya asilimia 11.

Grafu inayoonesha asilimia ya uwakilishi wa wanawake katika bunge la sasa la Ujerumani kwa vyama.

Kwa mujibu wa Lukoschat, hatua kuelekea usawa zaidi kati ya wanawake na wanaume katika siasa ingekuwa kupitisha sheria ya uwiano. Sheria kama hiyo inaweza kwa mfano, kuvitaka vyama vya siasa kutenga asilimia 50 ya nafasi za kwenye orodha au hata ugombea wa moja kwa moja kwa ajili ya wanawake.

"Nchini Ufaransa, sheria ya 'Loi sur la parité' imehakikisha kwamba uwiano wa wanawake bungeni unaongezeka," anasema mtafiti wa masuala ya jinsia Barbara Holland-Cunz kutoka chuo kikuu cha Giessen. Katika orodha ya wawakilishi wa kike mabungeni duniani, Ufaransa, katika nafasi ya 14 kati ya mataifa 193, iko katika nafasi bora zaidi kuliko Ujerumani, inayoshika nafasi ya 46.

"Mtazamo imara au ukali?"

"Imani yangu ya usawa wa kijinsia inaona hali ya sasa kuwa ya kutia wasiwasi, wanasayansi wanadhani tayari tumetoka safari ndefu. Lakini hali bado ni ile ile kwamba wanawake na wanaume hawachukuliwi kwa namna sawa katika uwanja wa siasa, hata kama wanafanya jambo sawa," anasema Holland-Cunz.

Ricarda Lang, msemaji wa tawi la vijana la chama cha Kijani, pia anakubaliana na tathmini yake. "Wanawake wanatazamwa haraka kama wakali, wababe au wapenda makuu pale wanapoelezea maoni mazito," anasema Lang. Hata katika chama cha Kijani, chenye zaidi ya asilimia 50 ya wawakilishi wanawake, anashuhudia hili: "Mtu hutatizwa mara kwa mara katika mikutano, au anatoa mchango wenye maudhui, ambao baadae unahusishwa na mwanaume. Swali muhimu hata hivyo ni iwapo chama kinanuwia kubadilisha hili au la," anasema.

Mwandishi: Marina Strauß

Tafsiri: Iddi ssessanga

Mhariri: Mohammed Khelef