1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tafrani nchini Ufaransa

Mjahida9 Januari 2015

Mwanamume mmoja aliyejihami kwa silaha amewachukua mateka watu kadhaa katika soko la kosher linalouza vyakula vya Kiyahudi, mashariki mwa mji mkuu wa Ufaransa Paris, tukio lililosababisha watu kadhaa kujeruhiwa.

Polisi washika doria Kaskazini Mashariki mwa Paris
Polisi washika doria Kaskazini Mashariki mwa ParisPicha: picture alliance/dpa/Jb Quentin

Watu wawili wameuwawa huku mmoja akijeruhiwa wakati mwanamume huyo aliyejihami kwa silaha alipoanza kuwamiminia risasi watu waliokuwa katika soko hilo la Kosher, Mashariki mwa Paris na kuwashikilia mateka watu watano. Hii ni kulingana na shirika la habari la AFP. Mshukiwa huyo ndiye anaedaiwa pia kuhusika na tukio jengine la mauaji ya polisi mmoja wa kike katika eneo la Montrouge Kusini mwa Paris.

Polisi inaendelea kumtafuta mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Amedy Coulibaly, mwenye umri wa miaka 32 na mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mpenzi wake Hayat Boumeddiene, mwenye miaka 26. Picha zao zimetolewa kwa umma na kuwataja kama watu hatari na waliojihami kwa silaha.

Kulingana na afisa mwingine wa polisi aliyezungumza na shirika la habari la AFP, mshambuliaji huyo anadaiwa kuwa na mahusiano na kaka wawili walioshambulia ofisi ya jarida la Charlie Hebdo siku ya Jumatano na kusababisha mauaji ya watu 12.

Polisi Ufaransa wakiwakamata watu waliokuwa na pikipiki waliosogelea soko la KosherPicha: Reuters/Y. Boudlal

Waliouwawa ni pamoja na waandishi habari wanane, maafisa wawili wa polisi, mfanyakazi mmoja na mgeni aliyetembelea ofisi hiyo siku ya tukio.

Hali hiyo imezidisha hofu kote nchini Ufaransa huku nchi hiyo ikiongeza hali ya tahadhari kwa mashambulizi ya kigaidi.

Ndugu wawili waendelea kusakwa na polisi

Kwengineko Kaskazini Mashariki mwa Paris Cherif Kouachi na Said Kouachi washukiwa wanaodaiwa kuhusika katika shambulio dhidi ya gazeti la Charlie Hebdo, wamezingirwa na polisi nje ya jengo moja wanamoaminika kujificha. Mbunge wa eneo hilo Yves Albarello, amesema washukiwa hao wanaoaminika pia kumshikilia mtu mmoja mateka, walimwambia mmoja ya watu waliokuwa wanawasiliana nao kuwa wanataka kufa mashahidi, yani kwaajili ya mwenyezi Mungu.

Vikosi vya usalama vimemuagwa katika mji huo mdogo wa viwanda wa Dammartin-en-Goele, karibu na uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle, baada ya washukiwa hao kuiba gari moja ya peugeot hii leo asubuhi, kabla ya kuishia katika jengo wanalozingirwa kwa sasa.

Helikopta zimeonekana angani huku maelfu ya polisi wakionekana katika eneo hilo. Serikali imewaomba wakaazi wa eneo hilo kubakia majumbani mwao wakati operesheni hiyo ikiendelea.

Washukia wa shambulio dhidi ya Charlie Hebdo Cherif Kouachi na Said KouachiPicha: picture-alliance/dpa/French Police/Handout

Kwa upande mwingine msemaji wa uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle amesema wamefunga njia mbili za kuingia ndege ili kutoingiliana na shughuli ya kuwatafuta washukiwa wa shambulio dhidi ya jarida la Charlie Hebdo, lililowahi kuchora kibonzo kilichomkejeli mtume wa dini ya Kiislamu Mtume Mohammad. Wakati wa shambulizi hilo siku ya Jumatano washukiwa hao walisema wamelipiza kisasi kufuatia kuchorwa kwa kibonzo hicho.

Cherif Kouachi alitiwa hatiani mwaka 2008 kwa makosa ya kuhusika katika visa vya ugaidi. Huku Said akisemekana kuwahi kusafiri nchini Yemen lakini haijulikani iwapo alitaka kujiunga na kundi la kigaidi la Al Qaeda nchini humo.Hata hivyo afisa mmoja wa Marekani amesema ndugu wote wawili walikuwa katika orodha ya watu waliopigwa marufuku kuingia nchini Marekani.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Iddi Ssessanga