Taiwan yaionya China kwa kurusha ndege za kivita
18 Septemba 2023Taiwan imetoa wito kwa China hivi leo kuachana na kile ilichotaja kuwa "hatua za uharibifu", baada ya zaidi ya ndege 100 za kivita na meli tisa za jeshi la wanamaji za China kuripotiwa katika maeneo yaliyo karibu na kisiwa hicho kinachojitawala.
Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema idadi ya ndege za kivita zilizoripotiwa ndani ya saa 24 ni kubwa mno huku Beijing hadi sasa ikijizuia kuelezea chochote juu ya tukio hilo.
Hatua hizo huenda ikawa jaribio la kuathiri matokeo ya uchaguzi wa rais unaotarajiwa mwezi Januari mwaka ujao.
China inawapigia upatu wagombea wa upinzani wenye dhamira ya kushirikiana na Beijing kuliko wale wa chama tawala cha DPP ambao sera yao inajikita katika uhuru kamili wa kisiwa hicho.
China inadai kuwa kisiwa cha Taiwan ni eneo lililo chini ya himaya yake na iwapo italazimika itakitwaa kwa nguvu. Beijing imekuwa ikiongeza shinikizo la kidiplomasia na kijeshi kwa Taipei katika miaka ya hivi karibuni.