1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaTaiwan

Taiwan yasema walinzi wa Pwani China wananyanyasa wavuvi

4 Julai 2024

Taiwan imeituhumu China kwa kunyanyasa moja ya boti zake za uvuvi kwenye bahari karibu na visiwa vya Penghu, siku moja baada ya Beijing kuikamata meli ya Taiwan kwa madai ya "uvuvi haramu".

Mzozo wa Taiwan na China
Taiwan yasema walinzi wa Pwani ya China wananyanyasa wavuviPicha: Chiang Ying-ying/AP Photo/picture alliance

Walinzi wa Pwani ya Taiwan wamesema walituma meli tatu za doria Jumatano jioni baada ya wito kutoka kwa boti ya wavuvi iliyokuwa ikiandamwa na idadi isiyojulikana ya meli za walinzi wa pwani ya China.

Walinzi hao wa Pwani wa Taiwan wamesema kisa hicho kilitokea umbali wa kilomita 111 Kaskazini Magharibi mwa Penghu, kisiwa cha mkono bahari wa Taiwan.

Soma pia: Kiongozi wa Taiwan asema China haina haki ya ´kuwaandama´

Tukio hilo linakuja huku Taipei ikiitaka Beijing kuiachilia mara moja boti ya wavuvi iliyowabeba raia wawili wa Taiwan na watatu wa Indonesia waliokamatwa na walinzi wa pwani ya China karibu na visiwa vya Kinmen vya Taiwan.

Kulingana na msemaji wa walinzi wa Pwani ya China, boti hiyo inayoshukiwa kufanya uvuvi haramu katika pwani ya Quanzhou kwenye jimbo la Fujian nchini China, ilikaguliwa na kuzuiliwa siku ya Jumanne.