Tajani aongoza kura ya Uspika wa bunge la Ulaya
17 Januari 2017Tajani ameshinda kura 274 kati ya kura zote zilizopigwa 683 zinazomuweka mbele ya mgombea mwengine wa siasa za mrengo wa kushoto wa wastani Gianni Pittella ambaye alipata kura 183. Wagombea wengine wanne walipata kati ya kura 43 na 77.
Iwapo hamna mgombea atakayepata wingi wa kura baada ya duru mbili za upigaji kura za Jumanne, wagombea wawili watakaoongoza kwa kura watashindana kwa duru ya nne na ya mwisho, Jumanne ijayo.
Kujiondoa kwa, Guy Verhofstadt, katika dakika za mwisho za kinyang'anyiro hicho, aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa Ubelgiji, kabla ya kura kuanza, kumemuongezea nguvu Tajani na kudhihirisha namna vyama vya kisisasa vinavyounga mkono kuwepo kwa Umoja wa Ulaya vinavyojaribu kuviziba sauti vyama vichache vinavyoukosoa na kuupinga umoja huo.
Bunge la Ulaya linashika nafasi kubwa katika kufanya maamuzi ya kuidhinisha sheria za Umoja huo ikiwa ni sehemu ya utawala wa mihimili mitatu unaojumuisha Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inayohusika na utendaji pamoja na Braza la Umoja wa Ulaya la nchi wanachama.
Verhofstadt, muumini mkubwa wa sera ya mfumo wa shirikisho ambaye pia amechaguliwa kuuwakilisha upande wa bunge la Ulaya katika majadiliano kuhusu Uingereza kujitenga na umoja huo, Brexit, ametaja baadhi ya changamoto inazozikabili umoja huo ikiwa ni pamoja na uhasama kutoka kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na rais mteule wa Marekani Donald Trump.
Kura hiyo imeleta utata usiokuwa wa kawaida tokea kundi la siasa za mrengo wa kushoto wa wastani la Wasoshalisti na Wahafidhina (S&D)- ambalo ni la pili kwa ukubwa baada ya chama cha siasa za mrengo wa kulia za wastani European People's Party (EPP)- kuvunja muungana na kundi hilo la EPP na lile la kileberali ili kusimamisha mgombea wake pekee wa kuwania wadhifa wa Rais Martin Schulz.
Awali kundi la S&D lilikubali - wakati mgombea wake Schulz alipochaguliwa kwa mara nyengine 2014 kwa usaidizi wa EPP- kuwa mara hii litamsaidia mgombea wa chama cha EPP. Mpasuko huo unaonekana kama njia ya kuupa sauti kubwa upande unaopinga kuwepo Umoja wa Ulaya uliochochewa na kura ya maoni ya Uingereza iliyopigwa mwaka jana na kuamua kujiondoa katika umoja huio.
Hali hiyo inaweza ikawapa ushawishi mkubwa wanasiasa wanaopinga Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Marine Le Pen na chama chake cha French National Front pamoja na Nigel Farage, wa Uingereza ambaye alipiga kampeni kubwa ya kushadidia taifa hilo kujitoa katika Umoja wa Ulaya pamojana ujumbe wake wa wanasiasa 20 wa chama cha Independence.
Hata hivyo jitihada za EPP sasa zinalenga zaidi katika kulivutia kundi la wahafidhina na wanamageuzi la European Conservative and Reformists (ECR), ambalo mgombea wake ameshika nafasi ya tatu katika kinyanga'nyiro hicho cha kugombea uspika wa Bunge la Ulaya. Likiongozwa na wanachama wa chama tawala cha kihafidhia cha Uingereza pamoja na chama tawala cha Poland cha siasa za mrengo wa kulia PiS, kura za kundi la ECR zinaweza kumsogeza katika ushindi Tajni.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre
Mhariri: Josephat Charo