1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takriban wanafunzi 100 hawajulikani walipo, Congo

Admin.WagnerD17 Desemba 2020

Mapigano kati ya makundi ya wanamgambo kwenye mkoa wa Maniema katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, yamesababisha raia kukimbilia vijiji jirani na eneo hilo huku wanafunzi takriban 100 wakiwa hawajulikani waliko. 

Ruanda-Rebellen von Sylvestre Mudacumura befehligt
Picha: AFP/L. Healing

Mapigano kati ya makundi ya wanamgambo yaliotokea kwenye mkoa wa Maniema katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,yamesababisha wakaazi wa Kabambare katika mkoa huo kukimbilia katika vijiji jirani na eneo hilo huku wanafunzi takriban 100 wakiwa hawajulikani waliko. 

Takriban wanafunzi 100 hawajulikani waliko huku vijiji kadhaa vikichomwa moto wakati wa mapigano kati ya makundi ya wanamgambo yaliotokea katika eneo la  Kabambare katika mkoa wa Maniema nchini Kongo. Taarifa hizo ni kulingana na redio Okapi inayomilikiwa na Umoja wa Mataifa.

Gavana wa Maniema, Auguyi Musafiri amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo akisema kwamba makundi hayo ya wanamgambo yalipigana karibu na shule moja iliyoko karibu, hatua iliyosababisha wanafunzi hao kutoroka.

Soma Zaidi:Watu kumi wauawa na waasi mashariki mwa DRC 

Gavana Musafiri amesema bado anafanya kazi na maafisa wake wa usalama kujua ni watoto wangapi hasa waliopotea na ni wangapi ambao mpaka sasa wamepatikana kutokana na taarifa kuwa baadhi yao walifanikiwa kurejea nyumbani.

Baadhi ya wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Taifa hilo linaendelea kukabiliwa na uasi unaosababisha raia kukimbia.Picha: picture-alliance/dpa/AFP/E. Goujon

Mapigano hayo yaliyotokea kwenye barabara inayotoka Kabambare kuelekea Kulerwa kuanzia tarehe 10 Desemba hadi tarehe 15 yamewalazimisha pia wakaazi wa eneo hilo kutafuta hifadhi katika vijiji vilivyoko karibu na eneo la tukio.

Gavana Auguyi Musafiri amesema maafisa wa polisi bado wako chonjo kudhibiti mashambulio mengine kama hayo yaliomalizika siku ya Jumanne na bado inaendelea na msako wa wanafunzi waliopotea.

Eneo la Kabambare ni eneo tajiri kwa dhahabu nchini Kongo na Shirika la kudhibiti mizozo ya kimataifa, ICG limesema kuwa ushindani baina ya kampuni kubwa za kuchimba migodi na wachimbaji wadogo wadogo wa madini husababisha mifarakano ya mara kwa mara nchini humo.

Hali kadhalika, Umoja wa Mataifa unasema kuwa unyonyaji wa raslimali asili za Kongo ni kigezo kingine cha migogoro isiyokoma upande wa mashariki wa nchi hiyo. Taifa hilo la Afrika ya Kati limekuwa likipambana na mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya wanamgambo kwa takriban miongo miwili.

Makundi mengi ya wanamgambo yameweka kando matakwa yao ya kisiasa na yanajihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa madini.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW