1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China: Tetemeko la ardhi lasababisha vifo vya watu 118

19 Desemba 2023

Tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu Kaskazini Magharibi mwa China, limesababisha vifo vya takriban watu 118. Hili ni tetemeko baya zaidi kutokea katika taifa hilo katika muda wa miaka 10

Tetemeko la ardhi katika mkoa wa Gansu ulioko Kaskazini Magharibi mwa china lililosababisha vifo ya takriban watu 118 Desemba 19.12.2023
Tetemeko la ardhi katika mkoa wa Gansu nchini ChinaPicha: Ma Xiping/Xinhua/dpa/pictue alliance

Waokoaji katika maeneo ya mashambani Kaskazini-Magharibi mwa China wamechimba katika vifusi vya nyumba zilizoporomoka leo baada ya tetemeko hilo la ardhi ili kutafuta manusura wa mkasa huo.

Soma pia:Zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha baada ya tetemeko la ardhi kupiga eneo la kaskazini magharibi mwa China

Maafisa katika mkoa wa Gansu wanasema tetemeko hilo lililotokea kabla ya saa sita usiku kuamkia leo, limesababisha vifo vya watu wasiopungua 105 na kujeruhi wengine takriban 400 kufikia leo asubuhi.

Tetemeko la ardhi laharibu maelfu ya nyumba

Watu wengine 13 walikufa, 182 walijeruhiwa na 20 hawajulikani walipo katika mji wa Haidong ulioko mkoa jirani wa Qinghai. Haya ni kulingana na ripoti za shirika la habari la CCTV.

Wakazi wakimbilia usalama katika maeneo ya barabara

Tetemeko hilo liliharibu maelfu ya nyumba nyingi zikiwa na miundo ya matofali na kuwafanya wakaazi kukimbilia usalama wao kwenye maeneo ya barabara .

Kanda za video za CCTV zilionesha mali za familia nyingi zikiwa zimetapakaa katika eneo hilo la tukio.

Kishindo cha tetemeko chasikika katika maeneo ya mbali na mkasa

Shirika la habari la China Xinhua liliripoti ukubwa wa tetemeko hilo la ardhi kuwa 6.2 katika kipimo cha ritcher na kusema kwamba mtikisiko huo ulisikika katika mji mkubwa wa Xi'an, ulio umbali wa kilomita 570.

Shughuli ya uokoaji na kutafuta manusura inaendelezwa katika mkoa wa GansuPicha: China Daily/REUTERS

Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa kufanywa kwa juhudi zote za kushughulikia hali hiyo wakati shughuli ya kutafuta manusura na uokoaji ikiendelezwa.

Bidhaa za msaada zapelekwa Gansu

Xinhua imeripoti kuwa bidhaa za msaada zinazojumuisha mahema 2,500, makoti 20,000 na vitanda 5,000 vimepelekwa Gansu, huku maji ya kunywa, blanketi, majiko na tambi pia zikisafirishwa kuelekea katika eneo hilo la mkasa.

Serikali kuu ya  China yatoa dola milioni 28 za msaada

CCTV imeripoti kwamba awali serikali kuu ilikuwa imetoa dola milioni 28 za ufadhili wa misaada ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali ya watu na pia kupunguza athari za hasara kutokana na maafa.

Rais wa Urusi Vladimiri Putin ametuma risala za rambirambi China

Huku hayo yakjiri, rais wa Urusi Vladimir Putin ametuma risala zake za rambirambi kwa mwenzake wa China kutokana na mkasa huo wa tetemeko la ardhi.

Katika taarifa kutoka ikulu ya Kremlin, Putin amesema kuwa nchini Urusi, wanashiriki katika machungu ya waliopoteza wapendwa wao na kuwatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa.