Mashambulio ya jeshi la Israel yauwa kiasi watu 200 Lebanon
9 Aprili 2026
Serikali ya Lebanon imetangaza siku ya maombolezo ya kitaifa kufuatia kuuwawa kwa karibu watu 200 kwenye mashambulio ya jana jumatano.
Hali ndani ya Lebanon inatisha kufuatia mashambulio makubwa yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel yakilenga maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.
Mashambulio ya Jumatano yalikuwa makubwa zaidi dhidi ya mji mkuu Beirut yakisababisha kuuwawa kwa watu karibu 200 na takriban 900 kujeruhiwa.
Israel imesema miongoni mwa waliouwawa ni pamoja na katibu na mpwa wa kiongozi wa Hezbollah,Naim Qassem, Ali Yusuf Harshi.
Serikali mjini Beirut imetangaza siku ya maombolezo ya kitaifa ikiagiza kushushwa kwa bendera nusu mlingoti na kufungwa kwa ofisi za serikali kutowa heshima kwa waliouwawa na kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo ya jeshi la Israel.
Israel yamuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa,Volker Turk amelaani kinachoendelea, kupitia msemaji wake Thameen al Kheetan.
"Kiwango cha mauaji na uharibifu nchini Lebanon ni cha kutamausha. Mashambulio yaliyofanywa saa chache baada ya kufikiwa ushitishaji vita na Iran, ni hatua inayoondowa imani. Inaleta shinikizo kubwa katika hali tete ya amani ,ambayo raia wanaohitaji. Idadi kubwa ya watu kuuwawa imeripotiwa na mahospitali yamefurika.Timu ya Haki za binadmu ya UN iliyoshuhudia imesimulia hali ya kutisha Beirut ikitaja kuona maiti nyingi chini ya vifusi.Juhudi za kuleta amani kwenye kanda nzima haziwezi kufanyikiwa ikiwa Walebanon wataendelea kushambuliwa, kuachwa bila makaazi na kubakia katika khofu ya kushambuliwa
Lakini pia Umoja wa Mataifa umelaani kwa maneno makali mashambulio ya Israel nchini Lebanon. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Stephen Dujjaric, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hali isiyo ya kawaida ametumia maneno makali kulaani mashambulio hayo yaliyofanywa na Israel baada ya kutangazwa kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita.
Ndege ya kivita ya Marekani yadunguliwa Iran, rubani mmoja aokolewa
Hata hivyo kumekuweko na ripoti za kutatanisha kuhusu makubaliano ya usitishaji vita,Israel ikisema makubaliano yaliyofikiwa hayahusishi vita vyake Lebanon dhidi ya Hezbollah,msimamo ambao pia umetolewa na Marekani japo Iran na Pakistan iliyosimamia mazungumzo hayo zimesema yanajumuisha pia Lebanon.
Vingora vilisikika kaskazini mwa Israel mapema hivi leo wakati kundi la Hezbollah likidai kufyetuwa maroketi kuelekea Israel.