1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takriban watu 40 wamekufa kutokana na mafuriko nchini Kongo

28 Desemba 2023

Takriban watu 40 zaidi wamekufa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha siku ya Jumanne kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi

Mafuriko katika eneo la Kisauni mjini Mombasa nchini Kenya, mnamo Novemba 17, 2023
Mafuriko mjini Mombasa nchini KenyaPicha: REUTERS

Mkazi mmoja wa Bukavu Yvonne Mukupi aliyenusurika mafuriko hayo, amesema jirani yake mmoja alisombwa na maji ya mafuriko. "Tumefanikiwa kupata miili mitatu chini ya miti lakini miili mingine bado haijapatikana, '' ameeleza Mukupi.

Vifo vyaripotiwa katika sehemu mbali mbali za Kongo

Takriban watu 20 walikufa katika eneo la Bukavu huku wengine takriban 20 wakipoteza maisha katika kijiji cha Burinyi, kilichoko umbali wa kilomita 50 kutoka Bukavu. Haya ni kwa mujibu wa maafisa katika maeneo hayo mawili.

Umoja wa Mataifa wasema mipangilio duni ya miundombinu inachangia kutokea kwa majanga

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa mipangilio duni ya miji na miundombinu dhaifu huzifanya baadhi ya jamii kuwa katika hatari zaidi ya kuathirika kutokana na mvua kubwa inayozidi kuongezeka na kunyesha mara kwa mara barani Afrika kutokana na ongezeko la joto.

Maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Nyamukubi Mashariki kwa KongoPicha: GLODY MURHABAZI/AFP

"Wakati kunaponyesha , njia kuu ya maji huziba wakati mwingine kwasababu ya taka na kusababisha mafuriko yanayoharibu nyumba,'' ameeleza afisa mmoja wa Bukavu Emmanuel Majivuno aliyekuwa katika eneo hilo la tukio wakati wakazi walipokuwa wakishughulika kuokoa mali yao kutoka kwa nyumba zilizoporomoka.

Tukio hilo linafuatia vifo vya takriban watu 22 katika jimbo la Kasai-Central siku ya Jumanne wakati maporomoko ya ardhi yalipofunika nyumba, makanisa na barabara, na kuua familia nzima huku baadhi ya watu wakiachwa bila makazi.