1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takriban watu nusu bilioni hawana kazi nzuri ulimwenguni: UN

21 Januari 2020

Watu milioni 470 ulimwenguni kote hawana ajira kabisa au hawana kazi nzuri ya kuwawezesha kujenga mustakabali bora. Hayo ni kulingana na ripoti ya kila mwaka ya Shirika la Kazi Duniani ILO.

Südafrika  South African Airways Streik
Picha: Reuters/S. Sishi

Umoja wa Mataifa umesema kuwa watu milioni 470 kwa sasa ulimwenguni kote hawana ajira kabisa au wameajiriwa chini ya kiwango. Kwenye ripoti yao iliyotolewa jana Umoja huo umeonya kuwa ukosefu wa ajira bora unachangia machafuko katika jamii.

Kwenye ripoti yake ya kila mwaka kuhusu ajira na tathmini ya jamii, Shirika la Kazi Duniani, ILO, limesema Mwaka huu, idadi ya watu ambao wamesajiliwa kuwa hawana ajira inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 188 mwaka uliopita hadi milioni 190.5.

Mnamo mwaka uliopita, zaidi ya watu milioni 630, ikiwa ni asilimia 20 ya idadi jumla ya wanaofanya kazi ulimwenguni, walitegemea kazi ya kijungu jiko, yaani kipato ni chini ya dola 3.20 kila siku.

Ripoti ya ILO imeonyesha kuwa asilimia 60 ya nguvu kazi ulimwenguni kote kwa sasa ni wale wanaofanya kazi zisizo rasmi, ambapo malipo ni kidogo na hawapati marupurupu muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, mkuu wa ILO Guy Ryder, amesema hali inazidi kuwa ngumu kwa mamilioni ya wale wanaofanya kazi, kuboresha maisha ya wengine kupitia ajira.

Vijana milioni 267 hawako kwenye ajira

"Vijana wanakabiliwa na changamoto za soko la ajira. Na kuna takwimu ya kushangaza kwenye ripoti hii. kuwa asilimia 22 ya vijana, milioni 267 hawako kwenye ajira, elimu au mafunzo ya kazi. Na hili ninafikiri ni changamoto kubwa katika enzi hizi zetu."

Ameonya kuwa kuendelea kuwepo kwa ukosefu wa usawa kuhusu masuala yanayofungamana na ajira pamoja na kutengwa, kunawazuia wengi kupata kazi nzuri ili waweze kujenga mustakabali bora.

Asilimia 60 ya nguvu kazi ulimwenguni kote kwa sasa ni wale wanaofanya kazi zisizo rasmiPicha: DW/S. Olukoya

Kuhusu mishahara, Ryder amesema kuna pengo kubwa kati ya wanaolipwa mishahara minono na wanaolipwa kidogo.

Pengo kubwa kati ya wenye mishahara minono na wanaolipwa kijungu jiko

Ripoti hiyo imegundua kuwa inawachukua takriban muda wa miaka 11 kwa asilimia 20 ya watu wenye kipato cha chini kupata kipato sawa na kile asilimia 20 ya wanaolipwa vizuri hupata katika mwaka mmoja pekee.

Wakati huo huo, shirika hilo limesisitiza kuwa takriban watu milioni 285 ulimwenguni kote, wanachukuliwa kama ambao hawajaajiriwa chini ya kiwango. Kumaanisha wanafanya kazi kidogo kuliko wanavyotaka kufanya au, wamekata tamaa kutafuta kazi, au wameshindwa kupenyeza katika soko la ajira.

ILO imeongeza kuwa kwa jumla hiyo ni takriban watu nusu bilioni, na inawakilisha asilimia 13 ya nguvu kazi kote duniani.

Ryder amesema ripoti hiyo imefichua hali mbaya zaidi ya kutia wasiwasi, huku akiongeza kuwa kukosa kazi nzuri ya kufanya, kunachangia kuongezeka kwa makundi ya waandamanaji katika jamii na machafuko yanayotokea ulimwenguni.

Amesema masharti katika soko la ajira yamechangia  mmomonyoko wa umoja wa jamii kwa njia  nyingi, akizungumzia maandamano makubwa kama ambayo yameshuhudiwa Lebanon na Chile.

Vyanzo: AFPE, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW