Taliban: Haki za wanawake wa Afghanistan ni suala la ndani
29 Juni 2024Tamko hilo limetolewa kuelekea mkutano unaoongozwa na Umoja wa Mataifa kujadili hali ya Afghanistan ambako suala la kutowajumuisha wanawake katika mkutano huo limekosolewa vikali.
Serikali hiyo ya Taliban iliyowawekea vikwazo wanawake tangu ilipochukua madaraka mwaka 2021, itatuma wajumbe wake katika mazungumzo ya duru ya tatu yatakayofanyika Qatar kuanzia kesho Jumapili.
Wawakilishi wa mashirika ya kiraia yakiwemo mashirika ya kutetea haki za wanawake watahudhuria mkutano huo wa kesho. Wawakilishi hao baadaye wanatarajiwa kuwa na mkutano mwengine na wajumbe wa kimataifa wakiwemo maafisa wa Umoja wa Mataifa baada ya kumaliza mkutano wao rasmi.
Makundi hayo yamekosoa hatua ya kutowajumuisha wanawake wa Afghanistankatika mkutano huo na kutokuwepo kwa masuala ya haki za binaadamu katika ajenda.
Hata hivyo msemaji wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Kabul kwamba serikali inatambua masuala ya wanawake, ambayo ni mamabo yanayopaswa kujadiliwa na waafghanistan wenyewe.