1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban kutangaza serikali mpya ya Afghanistan

3 Septemba 2021

Kundi la Taliban linajiandaa kutangaza serikali mpya Ijumaa huku dunia ikusubiri kwa shauku kuona iwapo utawala mpya utatimiza ahadi zao kwa Afghanistan.

Afghanistan | Mullah Baradar Akhund
Picha: Social Media/REUTERS

Duru kutoka kwa kundi hilo la Taliban zimesema leo kuwa mwanzilishi mwenza wa kundi hilo Mullah Baradar ataiongoza serikali hiyo mpya ya Afghanistan itakayotangazwa hivi punde. Kulingana na duru hizo, Baradar, anayeiongoza ofisi ya kisiasa ya kundi hilo la Taliban ataungana na Mullah Mohammad Yaqoob, mwanawe mwanzilishi mwenza wa kundi hilo marehemu Mullah Omar na Sher Mohammad Abbas Stanekzai katika nyadhifa kuu za serikali.

Taarifa nyingine zimesema kuwa Haibatullah Akhunzada, kiongozi mkuu wa kidini wa kundi hilo la Taliban atasimamia masuala ya kidinina uongozi katika mfumo wa kiislamu. Mmoja wa maafisa wa kundi hilo aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba viongozi wote wakuu wamewasili mjini Kabul ambapo maandalizi ya kuitangaza serikali mpya yanakaribia kukamilika.

Wapiganaji wa Taliban wakishika doria mjini KabulPicha: West Asia News Agency/REUTERS

Wakati huo huo, Wataliban wamewachagua maafisa wao wa usimamizi katika majimbo na maeneo kadhaa nchini Afghanistan na taasisi za serikali zimeanza polepole kufanya shughuli zake. Uvumi umeenea kuhusu muundo wa serikali hiyo mpya, ingawa mapema wiki hii, afisa mmoja mkuu alisema kuwa wanawake walikuwa na uwezekano wa kutojumuishwa.

Wanawake wafanya maandamano mjini Herat

Katika mji wa Herat, wanawake wapatao 50 walifanya maandamano katika barabara za mji huo hapo jana katika tukio lisilokuwa la kawaida kutetea haki ya kufanya kazi na kushirikishwa katika serikali hiyo mpya. Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa wanawake hao waliandamana huku wakiimba kuwa ni haki yao kupata elimu, kazi na usalama na kwamba hawaogopi na pia wameungana.

Mmoja wa waandaji wa maandamano hayo Basira Taheri, ameliambia shirika hilo la habari kwamba analitaka kundi hilo la Taliban kuwajumuisha wanawake katika baraza jipya la mawaziri. Haki za wanawake halikuwa suala kuu la kipekee lililoibua wasiwasi kuelekea tangazo hilo la Taliban la kuundwa kwa serikali mpya. Mjini Kabul, wakazi walielezea wasiwasi kuhusu changamoto za kiuchumi za muda mrefu nchini humo ambazo sasa zimeongezeka kutokana na hatua ya kundi la Taliban kuchukuwa uongozi wa nchi hiyo.

Mapema wiki hii, Umoja wa Mataifa ulionya kuhusu uwezakano wa kutokea kwa mzozo wa kibinadamu nchini Afghanistan, ukitoa wito kwa wanaotaka kuutoroka uongozi huo mpya kuruhusiwa kufanya hivyo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW