Taliban na Afghanistan wajadili kuachiwa kwa wafungwa
23 Machi 2020Pande hizo mbili zimetofautiana kuhusu kuachiwa kwa wafungwa hao ambapo serikali inataka kuwaachia kwa awamu huku Taliban ikitaka wafungwa wote kuachiwa mara moja kama ilivyoafikiwa katika makubaliano na Marekani mjini Doha mwezi uliopita.
Mkwamo huo umetishia kurejesha nyuma mchakato wa amani uliojadiliwa kwa umakini kama ilivyoainishwa katika makubaliano hayo yanayojumuisha kuondolewa kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni kutoka Afghanistan baada ya zaidi ya miaka 18 ya mapigano.Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Afghanistan Zalmay Khalilzad amesema kuwa pande hizo mbili zilizungumza kwa zaidi ya masaa mawili kupitia mtandao wa Skype katika mkutano uliowezeshwa na Marekani naQatar.
Khalizad aliongeza kuwa kila mtu anafahamu kwamba tishio la virusi vya corona linafanya suala hilo la wafungwa kuwa la dharura na kwamba pande hizo mbili zilielezea dhamira yao katika kupunguza ghasia, kufanya mazungumzo ndani ya Afghanistan na makubaliano makhsusi ya kusitisha kabisa mashambulizi.
Makubaliano hayo yaliotiwa saini na Khalilzad na afisa mmoja mkuu wa Taliban mnamo Februari 29 mjini Doha, yaliweka msingi wa kuhitimisha vita vya muda mrefu vya Marekani vilivyoanza baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001.Makubaliano hayo, yaliafikia kuachiliwa huru kwa wapiganaji wanaofikia elfu 5 wa Taliban wanaozuiliwa mjini Kabul na hadi wanachama elfu 1 wa vikosi vya kijeshi la serikali walioko mikononi mwa kundi hilo la wanamgambo.
Hatua hiyo ilipaswa kuchukuliwa kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo ya amani kati ya serikali ya Afghanistan ambayo haikuwa sehemu ya mazungumzo yaliosababisha kupatikana kwa makubaliano ya Doha na Taliban ambayo awali yalikuwa yafanyike Machi 10.Awali serikali ya Afghanistan ilikataa mpangilio huo. Inaripotiwa kuwa rais Ashraf Ghani alikasirishwa na sharti la kuachiwa kwa wafungwa na kusema ni serikali pekee iliyo na uwezo wa kuidhinisha hatua kama hiyo.
Hatimaye alikubali mpango huo wa kuachiwa kwa wafungwa lakini kwa awamu na kusema hili lingefanyika tu iwapo ghasia zingepunguzwa. Msemaji wa baraza la kitaifa la usalama nchini Afghanistan Javid Faisal, amesema wanahitaji hakikisho kwamba hawatarejea katika vita.
Hata hivyo kundi la Taliban limesema kuwa liko tayari kwa awamu inayofuata ya mazungumzo ya amani lakini halitakutana na maafisa wakuu wa serikali hadi wakati wafungwa wao watakapoachiliwa huru. Maafisa wa serikali wameripoti kuwa tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya Doha, wanamgambo wametekeleza mashambulizi kadhaa. Wanamgambo waliovamia kituo cha polisi katika mkoa wa Kusini wa Zabul siku ya Ijumaa waliwauwa takriban maafisa 24 wa polisi na wanajeshi.