1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban waanzisha mashambulizi nchi nzima

4 Mei 2021

Baada ya wanajeshi wa Marekani kushindwa kuzingatia tarehe ya mwisho ya kuondoka Afghanistan ya Mei Mosi Taliban wameanzisha operesheni kubwa ya kijeshi nchi nzima

Symbolbild Kämpfe Afghanistan
Picha: Saifurahman Safi/Xinhua/picture alliance

Vikosi vya usalama  nchini Afghanistan vimeingia kwenye mapambano dhidi ya Taliban walioanzisha  operesheni kubwa ya kijeshi katika mkoa wa kusini wa Helmand ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Maafisa na wakaazi wameyasema hayo leo Jumanne katika wakati ambapo wanamgambo wa Taliban wameanzisha hujuma katika maeneo mbali mbali ya nchi nzima,baada ya Marekani kushindwa kutekeleza makubaliano ya kuwataka wanajeshi wake waondoke kufikia tarehe ya mwisho ya Mei Mosi.

Japo Marekani haikutimiza ahadi ya kuondoa wanajeshi wake kufikia Mei Mosi kama ilivyokubalika katika mazungumzo na Taliban mwaka jana,nchi hiyo imeanza kuondowa wanajeshi wake,huku rais Joe Biden akitangaza kwamba wanajeshi wake wote watakuwa wameondoka kufikia Sept 11.

Wakosoaji wa uamuzi huo wa kuondowa wanajeshi Afghanistan wanasema wanamgambo hao watajaribu kurudi tena madarakani. Attaullah Afghan, ambaye ni mkuu wa baraza mkoa wa Helamand amesema Taliban walianzisha operesheni kubwa jana Jumatatu kutokea maeneo mbali mbali wakishambulia vituo vya ukaguzi wa usalama katika eneo la kuzunguuka mji wa  Lashkar Gah na kuviteka baadhi ya vituo hivyo.

Picha: Sanaullah Seiam/XinHua/dpa/picture alliance

Vikosi vya usalama vya Afghanistan vilianzisha mashambulizi ya anga na kupeleka kikosi maalum cha  komando katika eneo hilo.Mulah Jan, mkaazi wa mji mkuu wa Helamnd,Lashkar Gah amesimulia kwamba kulikuwa na wimbi kubwa la mashambulizi na milio ya silaha nzito nzito na miripuko katika mji huo na milio ya silaha ndogo zilizosikika,mithili ya bisi zinapokaangwa.

Mkaazi huyo anasema aliichukua familia yake nzima kwenye kona moja ya chumba walikojibanza wakisikiza milio ya silaha nzito na risasi ambazo zilisikika kama vile zinafyetuliwa nje ya ukuta wa nyumba yao.

Imeelezwa kwamba familia zilizoweka kumudu kuondoka zimekimbia lakini mkaazi huyo ameshindwa kwenda kokote na amelazimika kusubiri pamoja na familia yake wakiwa na hofu kubwa,kabla ya wapiganaji wa Taliban kuzidiwa nguvu na kutimuliwa.

Picha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Athari ya kujiimarisha Taliban

Kuongezeka Taliban katika mkoa wa Helmand kutakuwa na athari mahsusi kutokana na mji huo kuwa mkulima mkubwa wa zao la Opium ambako ndiko wanajeshi wa Marekani na Uingereza walipata pigo kubwa katika vita ya miaka 20 nchini humo.

Kama sehemu ya kuondoka,vikosi vya wanajeshi wa Marekani viliikabidhi kambi yake ya Helmand kwa wanajeshi wa Afghanistan siku mbili zilizopita.Wizara ya ulinzi ya Afghanistan imesema kwamba pamoja na mkoa wa Helmand,vikosi vyake vya usalama vimekuwa vikijibu mashambulizi ya Taliban katika miko mingine takriban sita ikiwemo mkoa wa Kusini Mashariki wa Ghazni na Kusini mwa Kandahar ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wizara hiyo ya ulinzi imeeleza kwamba ni wapiganaji wataliban hadi 100 tu waliouwawa katika mkoa wa Helmand.Haikutowa maelezo kuhusu wanajeshi waliouwawa.

Picha: AFP/N. Mohammad

Mei mosi ilikuwa ndiyo tarehe ya mwisho iliyotolewa ya wanajeshi wa Marekani kuondoka Afghanistan chini ya makubaliano ya mwaka jana yaliyofikiwa chini ya utawala uliopita wa Marekani wa Donald Trump. Taliban wamelipinga tangazo la rais Biden kwamba wanajeshi wake wataondolewa taratibu katika kipindi cha miezi minne na nusu ijayo na sio wote kwa mpigo Mei Mosi.

Tarehe hiyo ya mwisho imeshuhudia ongezeko kubwa la vita ambapo mashambulizi ya bomu la kutegwa kwenye gari yamefanyika katika mkoa wa Logar na kiasi watu 30 waliuwawa siku ya ijumaa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri. Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW