1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wakamata eneo kubwa la Afghanistan

22 Julai 2021

Mkuu wa Baraza la Kijeshi Marekani Jenerali Mark Milley amesema kundi la Taliban linaonekana kuwa na muendelezo wa kimkakati katika mapambano ya kukamata udhibiti wa Afghanistan, wakati wakiiwekea shinikizo miji muhimu

US-Militär General Mark Milley
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Marekani Jenerali Mark Milley amesema kundi la Taliban linaonekana kuwa na muendelezo wa kimkakati katika mapambano ya kukamata udhibiti wa Afghanistan, wakati wakiiwekea shinikizo miji muhimu. Hatua hiyo inatengeneza mazingira ya kipindi kigumu katika wiki zijazo wakati wanajeshi wa Marekani wakikamilisha shughuli zao za kuondoka nchini humo. 

Soma pia: Mazungumzo ya Afghanistan yakamalika Doha bila ufumbuzi

Katika kikao cha waandishi wa habari kwenye makao makuu ya wizara ya ulinzi - Pentagon, Jenerali Milley amesema sasa utakuwa ni mtihani kwa dhamira na uongozi wa watu wa Afghanistan - vikosi vya usalama vya Afghanistan na serikali ya Afghanistan. "Wanachojaribu kufanya Mataliban ni kuyatenga maeneo muhimu ya mijini yenye watu wengi. Na wanajaribu kufanya hivyo mjini Kabul. Na kuhusiana na hali ilivyo, eneo kubwa la nchi limekamatwa na Taliban katika kipindi cha miezi 6, 8, 10 kitu kama hicho." Amesema Milley

Austin amesema Marekani itapambana na magaidiPicha: SARAH SILBIGER/newscom/picture alliance

Wizara ya Ulinzi imesema asilimia 95 ya wanajeshi wa Marekani wameondoka na shughuli hiyo itakamilishwa Agosti 31. Na wakati utawala wa Biden umeapa kuendelea kutoa msaada wa kifedha na vifaa kwa wanajeshi wa Afghanistan baada ya Agosti, Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin amesema jukumu litakalobaki kwa Marekani ni kusaidia kupambana na vitisho vya kigaidi, na wala sio Taliban. "Lengo letu kuu sasa katika kwenda mbele ni kuhakikisha kuwa, machafuko, ugaidi haviwezi kuhamishwa kutoka Afghanistan hadi kwenye nchi yetu." Amesema Austin.

Austin amesema Marekani imelikabidhi jeshi la Afghanistan helikopta tatu za kijeshi aina ya Blackhawk na kuwa vifaa zaidi vitafuata. Amesema wanajeshi wa Marekani wamewekwa Qatar kuendelea kupambana na magaidi Afghanistan baada ya kuondoka vikosi vya kigeni.

Soma pia: Taliban yadai kuudhibiti mji katika mpaka na Pakistan

Jenerali Miley amesema Wataliban sasa wanadhibiti zaidi ya nusu ya wilaya 419. Bado hawajakamata mji mkuu wowote kati ya mikoa 34 ya nchi hiyo lakini wameongeza shinikizo kwa karibu nusu ya miji hiyo. Matamshi yake yamekuja saa chache tu baada ya Taliban kusema jana kuwa watapigana tu ili kujilinda katika wakati wa sherehe za Eid al-Adha, lakini hawakutangaza rasmi mpango wa kusitisha mapigano.

Wanamgambo wa hao wa itikadi kali wanasema wanaunga mkono kwa dhati ufumbuzi wa kisiasa ili kumaliza vita vyao na serikali mjini Kabul. Lakini operesheni yao ya kutumia fursa iliyojitokeza kutokana na kuondoka kwa vikosi vya kigeni kumewaacha Waafghanistan wengi na wasiwasi. Rais Ashraf Ghani amesema Taliban imedhihirisha kuwa hawana dhamira ya amani na balozi kadhaa mjini Kabul zimetaka operesheni hiyo isitishwe mara moja.

AFP/DPA/AP/reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW