1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban waonya kuongezwa muda wa vikosi vya kigeni

23 Agosti 2021

Kundi la Taliban limetahadharisha kwamba kutakuwa na "athari" iwapo Marekani na marafiki zake wataongeza muda wa kuwepo kwa vikosi vyao nchini Afghanistan zaidi ya wiki ijayo.

Afghanistan Kabul | Taliban-Checkpoint
Picha: Rahmat Gul/AP/dpa/picture alliance

Akizungumza na shirika la habari la Sky News leo, msemaji wa Taliban Suhail Shaheen amesema kundi hilo halitokubali iwapo Marekani au Uingereza wataomba muda zaidi wa kuwaondoa watu nchini humo.

Mbio za kuikimbia Afghanistan zimesababisha vifo vya watu 8 huku wengine wakifariki kutokana na mkanyagano na mtu mmoja akiwa aliaga dunia baada ya kuanguka kutoka kwenye ndege iliyokuwa ikielekea kupaa.

Soma pia: Wataliban hawataongeza muda wa kuhamishwa watu

Wanamgambo hao pia wamewataka maimamu nchini humo kutoa hakikisho kwa raia kuhusiana na usalama wao. Zabihullah Mujahid ambaye ni msemaji wa muda mrefu wa Taliban katika mkutano na viongozi wa kidini amesema, ni jukumu la viongozi hao kuwatuliza raia wao.

Biden asema lengo ni kuwahamisha raia kwa wingiPicha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Mujahid pia amewataka waiondoe propaganda inayosambazwa na Marekani kuhusiana na kundi hilo na badala yake waiunge mkono serikali.

Haya yanafanyika wakati ambapo duru zimeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa kundi hilo la wanamgambo pia limesema halitotangaza serikali yake hadi Marekani itakapokamilisha kuyaondoa majeshi yake.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Saeed Khatibzadeh ametaka kuwepo na maelewano wakati wa kuundwa kwa serikali hiyo.

"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika mawasiliano ya mara kwa mara na pande zote za kisiasa Afghanistan. Historia ya Afghanistan inaonyesha matatizo ya nchi hiyo hayasuluhishwi kijeshi, kama ilivyokuwa tu majeshi ya Marekani yalipoingia nchini humo."

Soma pia: Marekani imejikita katika kuondoa vikosi vyake Afghanistan

Kwa sasa Taliban kupitia taarifa imesema imemteua kaimu mkuu wa benki kuu ya Afghanistan kusaidia kupunguza mzozo wa kiuchumi unaozidi nchini humo.

Haji Mohammad ndiye aliyeteuliwa kuishikilia nafasi ya gavana wa benki hiyo huku benki nchini humo pamoja na afisi za serikali zikiwa zimefungwa tangu wanamgambo hao kuchukua madaraka wiki moja iliyopita.

Ndege ya Ujerumani ikiwahamisha WaafghanistanPicha: Marc Tessensohn/Bundeswehr/dpa/picture alliance

Kuhusiana na suala la kuwaondoa raia walio katika hatari kubwa nchini humo, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian anatarajiwa kuwasili Falme za Kiarabu leo kujionea zoezi la kuwaondoa raia hao wa Afghanistan kwa kulitumia taifa hilo la Ghuba kama kituo.

Ufaransa inapania kuwahamisha zaidi ya raia elfu moja wa Afghanistan na Le Drian pamoja na ujumbe wake wanatarajiwa kuzuru kambi ya kijeshi ya Al-Dhafra iliyoko kilomita 30 kutoka Abu Dhabi, ambapo majeshi ya Ufaransa yamekuwa yakifanya harakati hizo za kuhamishwa kwa raia.

Soma pia: Afghanistan: Watu saba wafariki katika mtafaruku nje ya uwanja wa ndege wa Kabul

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Chung Eui-yong amewaambia wabunge kuwa Marekani imefanya mazungumzo ya awali na nchi hiyo kwa ajili ya kutumia kwa muda kambi zake ili kuwapa makao wakimbizi kutoka Afghanistan, ingawa mazungumzo hayo hayajapiga hatua.

Reuters/AP/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW