1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wasema wako tayari kuendelea na mazungumzo

29 Novemba 2019

Rais Donald Trump alifanya ziara ya ghafla nchini Afghanistan kukutana na wanajeshi wa Marekani na akasema kuwa anaamini kuwa Taliban watakubaliana kusitisha mapigano

US-Präsident Trump besucht Afghanistan
Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Brandon

((Taliban wamesema leo kuwa wako tayari kuanza tena mazungumzo na Marekani, siku moja baada ya Rais Donald Trump kufanya ziara ya ghafla nchini Afghanistan kukutana na wanajeshi wa Marekani na akasema kuwa anaamini kundi hilo la itikadi kali litakubaliana kusitisha mapigano. Bruce Amani ana mengi zaidi katika ripoti ifuatayo))

Ziara ya Trump katika Siku Kuu ya Kutoa Shukrani ilikuwa yake ya kwanza nchini Afghanistan tangu alipoingia madarakani na ilikuja wiki moja baada ya mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Marekani na Afghanistan ambao umeongeza matumaini ya kupatikana muafaka wa amani uliotafutwa kwa muda mrefu ili kumaliza vita vya miaka 18.

Tump alizungumza na wanahabari katika kambi ya jeshi la Marekani ya Bagram Airflied nje ya mji mkuu Kabul, baada ya kukutana na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani. "Taliban wanataka kufikia makubaliano na tunakutana nao na tunawaambia lazima uwe mpango wa kusitisha mapigano. Na hawakutaka kuweka chini silaha.  Lakini sasa ninaamimi wanataka kusitisha mapigano. Huenda ikawa hivyo. Na tutaona kitakachotokea. Lakini tumepiga hatua kubwa.

Trump alifanya mazungumzo na Rais Ashraf Ghani wa AfghanistanPicha: Reuters/T. Brenner

Viongozi wa Taliban wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kundi hilo limekuwa likifanya mikutano na maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani mjini Doha tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, akiongeza kuwa huenda hivi karibuni wakarejea tena katika mazungumzo rasmi ya Amani.

Hii leo, Zabiullah Mujahid, msemaji wa kundi hilo, amesema wako tayari kuanza tena mazungumzo hayo, ambayo yalivunjika baada ya Trump kuyasitisha mapema mwaka huu.

Trump alifuta mazungumzo ya Amani mwezi Septemba baada ya kundi hilo la wanamgambo kudai kuhusika na shambulizi la Kabul lililowauwa watu 12, akiwemo mwanajeshi wa Marekani.

Kamanda mmoja mwandamizi wa Taliban ambaye hajataka kutajwa jina, amesema wanatumai kuwa ziara ya Trump nchini Afghanistan itadhihirisha kuwa amedhamiria kuanzisha tena mazungumzo. Wanaamini kuwa Trump hana chaguo jingine.

Kwa sasa kuna wanajeshi 13,000 wa Marekani pamoja na maelfu ya wanajeshi wengine wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Afghanistan, miaka 18 baada ya uvamizi wa muungano ulioongozwa na Marekani kufuatia mashambulizi ya al-Qaeda nchini Marekani Septemba 11, 2001.

Karibu wanajeshi 2,400 wa Marekani wameuawa katika kipindi hicho cha vita. Rasimu ya muafaka uliofikiwa Septemba unawataka maelfu ya wanajeshi wa Marekani kuondoka kwa kuhakikishiwa kuwa Afghanistan haitatumika kama ngome ya kufanya mashambulizi nchini Marekani au washirika wake.

Maafisa wengi wa Marekani wanashuku kama Taliban inaweza kutegemea kuzuia alQaeda dhidi ya kupanga tena mashambulizi dhidi ya Marekani kutokea ardhi ya Afghanistan

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW