Taliban waua polisi Afghanistan
26 Aprili 2012Tukio hilo lilifanyika katika jimbo la Badakhshan usiku mzima huku wanamgambo hao wa Taliban wakipigana kwa kujiamini bila woga na kusababisha mauaji ya maafisa hao na wengine wawili wakijeruhiwa vibaya pamoja na maafisa watatu hawajulikani walipo.
Kulingana na taarifa za Gavana Msaidizi wa jimbo moja jirani na hapo Shamsul Rahman Shams anasema kulikuwa na mapigano makali katika eneo hilo katika milima ya Wardaj.
Gavana huyo ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa(AFP) akiwa katika mji wa Faizabad kuwa polisi walijaribu kujibu mashambulizi lakini Wataliban waliwazidi nguvu na kuwateka polisi na kuondoka nao kueleke mahala kusikojulikana.
Gavan Shams amehakikisha kuwa malori mawili ya polisi nayo yalitekwa yakiwa na shehena kubwa ya risasi iliyokuwamo katika magari hayo.
Taliban yapata msaada Asia ya kati
Eneo kulikofanyika mashambulio hayo kupo jirani na mpaka wa Pakistan, Tajikistan na China katika Asia ya kati. Kuna madai kuwa Wataliban hao wameweza kufanya shambulio hilo kwa msaada kutoka kwa askari wa mataifa ya Asia ya kati bila ya kutajwa nchi wanakotoka.
Jeshi la Afghanistan kwa sasa lina polisi 170,000, wakipewa mafunzo, vifaa na kulipwa mishahara na Marekani sambamba na Askari wa Marekani na wale wa Jumuiya ya Kujiami ya Ulaya (NATO) ambao kwa sasa ni 30,000. Jumla kukiwa na vikosi vya usalama vya askari laki mbili wanaopambana na Taliban.
Majeshi ya Marekani yamepanga kumaliza mpango wa kuondoka Afghanistan mwaka 2014 ambapo majukumu ya ulinzi na usalama wa taifa hilo yatakuwa chini ya Afghanistan yenyewe na inatarajiwa kuwa na Askari 352,000 mwaka huo.
Kwa mwaka huu kumefanyika mashambulio kadhaa ambayo kwa hakika yanatoa tashwira kuwa vikosi vya Usalama vya Jumuiya ya Kujiami ya Ulaya (NATO) pamoja na Marekani vimeshindwa kabisa kuleta amani nchini Afghanistan.
Mwandishi:Adeladius Makwega/AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman