Taliban wauteka mkoa mwingine tena Afghanistan
9 Agosti 2021Kutekwa kwa mji huo ndio tukio la hivi karibuni baada ya mashambulizi ya wiki nzima yaliyofanywa na kundi hilo wakati ambapo vikosi vya majeshi ya Marekani na Muungano wa kujihami wa NATO wakiwa wako katika hatua za mwisho za kuondoka nchini humo.
Kulingana na Mohammad Noor Rahmani, mkuu wa baraza la mkoa wa Sar-e Pul kaskazini, Taliban waliuteka mji mkuu wa mkoa huo baada ya mapambano makali ya wiki nzima na vikosi vya serikali ya Afghanistan. Rahmani anasema kwa sasa vikosi vyote vya serikali vimeshaondoka katika mkoa huo.
Sar-e Pul ni mojawapo ya mikoa mingine iliyotekwa
Mkuu huyo wa baraza la mkoa wa Sar-e Pul pia anasema wanamgambo wengine wanaoiunga mkono serikali pia wamejisalimisha kwa Taliban na kutoa nafasi kwa kundi hilo kuchukua udhibiti wa mkoa mzima. Sar-e Pul sasa unaingia kwenye hesabu ya miji mikuu ya mikoa ambayo kwa sasa iko kwenye udhibiti kamili wa Taliban. Mingine ni mji wa Zaranj ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Nimroz magharibi, mji wa Shibirghan ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Zawzjan na Taleqan ambao mkoa wake unaitwa Taleqan pia.
Lakini msemaji wa wizara ya usalama wa ndani ya Afghanistan Mirwais Stanikzai amesema majeshi ya serikali bado yanapambana katika mkoa wa Kunduz.
"Majeshi ya Afghanistan kwa ushirikiano na majeshi ya anga yameanza operesheni ya safisha safisha katika mji wa Kunduz. Majeshi hayo yanapiga hatua na yamechukua tena udhibiti wa sehemu kadhaa za mji huo na wanamgambo wengi wa Taliban wameuwawa. Karibuni mji huo hautokuwa na magaidi hao tena."
Idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi Afghanistan inaongezeka
Hayo yakiarifiwa wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa Taliban wamemuuwa meneja wa kituo cha redio katika mkoa wa kusini wa Helmand. Maafisa wa serikali ya mkoa huo wanasema hili ni mojawapo ya shambulizi ambapo waandishi wa habari wanalengwa.
Mwezi uliopita shirika moja la kutetea haki za binadamu linalounga mkono uhuru wa vyombo vya habari liliripoti kwamba waandishi 30 waliuwawa, kujeruhiwa au kutekwa nyara na makundi ya wanamgambo Afghanistan.
Kwengineko takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu masuala ya kiutu OCHA zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la wakimbizi wa ndani ya nchi tangu kuanza kuondoka kwa majeshi ya Marekani na NATO nchini Afghanistan.
Shirika hilo linasema karibu watu 244,000 wameyakimbia makaazi yao tangu mwanzoni mwa mwezi Mei wakati Taliban ilipoanza mashambulizi dhidi ya serikali ya Afghanistan.