Taliban wazidi kufagia miji Afghanistan, dunia yashtushwa
13 Agosti 2021Katika muda wa masaa 24, mji wa pili na wa tatu kwa ukubwa nchini Afghanistan - Herat ulioko magharibi na Kandahar ulioko kusini, imeangukia mikononi mwa waasi wa Taliban kama ilivyotokea kwa mji mkuu wa mkoa wa Helmand, ambako vikosi vya Marekani, Uingereza na Jumuiya ya kujihami NATO, vilipigana moja ya mapambano makali zaidi katika mzozo huo.
Soma pia: Taliban yaombwa kujiunga na serikali
Wapiganaji wa Taliban pia wameuteka mji mkuu wa mkoa wa Logar - Pul-e-Alam, ulioko umbali wa kilomita 50 tu kutoka Kabul. Mapema leo, maafisa na wakaazi mjini Kandahar, walisema vikosi vya serikali vilijiondoa kwa wingi na kukimbilia kambi ya kijeshi nje ya mji huo wa kusini mwa Afghanistan. Saa kadhaa baadae, Taliban wakasema wamechukua pia udhibiti wa Lashkar Gah, ambao ni mji mkuu wa mkoa jirani wa Helmand.
Kimsingi serikali sasa imepoteza sehemu kubwa ya nchi kufuatia kampeni kali ya kijeshi ya Taliban iliyodumu kwa siku nane tu na ambayo imeishtua hata Marekani, ambayo ni mfadhili mkuu wa serikali mjini Kabul.
Soma pia: Kundi la Taliban lauteka mji wa 10 Afghanistan
Umoja wa Mataifa sasa unatahadharisha juu ya mzozo mkubwa wa kibinadamu unaoinyemelea nchi hiyo. "Mzozo huu umeongezeka kwa kasi kubwa sana kuliko tulivyotarajia, na hali ina viashiria vya janga la kibinadamu," amesema Thomson Phiri, msemaji wa shirika la chakula la umoja huo WFP.
Wimbi la kwanza la mashambulizi lilianzishwa mapema mwezi Mei baada ya Marekani na washirika wake kuondoa vikosi vyao kutoka Afghanistan, huku rais Joe Biden akisistiza dhamira yake ya kumaliza miongo mwili ya vita kufikia Septemba Mosi.
Nguvu yaelekezwa mijini
Mzozo huo umeongezeka pakubwa tangu mwezi Mei, wakati vikosi vinavyoongozwa na Marekani vilipoanza hatua ya mwisho ya kuondoa wanajeshi wake. Baada ya miezi kadhaa ya kuchukuwa kile kilichodhaniwa kuwa maeneo ya vijijini yasio ya kimkakati, Talibani wakaelekeza nguvu na mawazo yao kwenye miji.
Waasi hao wamechukua zaidi ya dazen moja ya miji mikuu ya mikoa katika wiki moja iliyopita na kuuzingira mji mkubwa zaidi eneo la kaskazini, katika ngome ya asili ya upinzani dhidi ya Taliban wa Mazar-i-Sharif, ambao hivi sasa ni moja ya michache inayoendelea kutoa upinzani.
Soma zaidi:Afghanistan: Mikoa zaidi yaingia mikononi mwa Taliban
Uingereza hii leo imekosoa hatua ya Marekani kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan, na kusema kuwa kurudi kwa Taliban kutatengeneza mazingira kwa makundi ya itikadi kali yanayoitishia dunia.
Chanzo: Mashirika