1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yaombwa kujiunga na serikali

12 Agosti 2021

Wajumbe wa serikali ya Afghanistan kwenye mazungumzo ya amani nchini Qatar wamewapa mapendekezo Wataliban ya uwezekano wa kugawana madaraka ili kusitisha mapigano nchini humo.

Afghanistan Präsident Ashraf Ghani
Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Mjumbe mmoja wa  serikali ya Afghanistan katika mazungumzo hayo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa, amesema kuwa wakati vikosi vya serikali vikiendelea kuondoka katika maeneo mengi nchini humo, serikali ya nchi hiyo imetoa pendekezo hilo kwa kundi la Taliban ili kusitisha mapigano. Mjumbe mwengine, Ghulam Farooq Majroh naye amesema kuwa kundi hilo la Taliban limepewa pendekezo hilo kuhusu serikali ya amani bila ya kutoa maelezo halisi.

Haya yanatokea wakati wanamgambo wa Taliban leo wakiuteka mji mwengine mkuu wa mkoa wa Ghazni ulioko kilomita 130 kusinimagharibi mwa Kabul, huu ukiwa ni mji wa kumi uliotekwa na waasi hao katika kipindi cha mashambulizi ya wiki nzima kote Afghanistan. Kutekwa kwa mji wa Ghazni ni pigo jengine kwa majeshi ya serikali ya Afghanistan kwani jambo hili litauwekea mji mkuu Kabul shinikizo zaidi. Huku uwezo wa serikali ya Afghanistan kufanya mashambulizi ya angani ukiwa ni mdogo, jeshi la anga la Marekani linaaminika limekuwa likifanya mashambulizi kuyaunga mkono majeshi ya serikali.

Wapiganaji wa kundi la Taliban mjini GhazniPicha: Gulabuddin Amiri/AP Photo/picture alliance

Hii leo, Ujerumani imesema kuwa itakatiza msaada wa kifedha kuelekea Afghanistan iwapo kundi la Taliban litafanikiwa kutwaa mamlaka nchini humo. Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani ZDF, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema kuwa kundi la Taliban linafahamu kwamba Afghanistan haiwezi kuendeleza shughuli zake bila msaada wa kimataifa.

Ujerumani hutuma msaada wa dola milioni 504 kila mwaka nchini Afghanistan na kulifanya taifa hilo kuwa mmoja wa wafadhili wakubwa zaidi katika taifa hilo.

Wakati huo huo Ufaransa imesitisha zoezi la kuwarudisha nyumbani wahamiaji kutoka Afghanistan kutokana na hali ya usalama kuzidi kuwa mbaya. Msemaji wa wizara ya Mambo ya Ndani amesema Ufaransa na washirika wake wa Ulaya wanafuatilia kwa makini hali nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa taarifa wapiganaji wa Taliban wanasonga mbele katika mapambano ya kuichukua Afghanistan yote. Mashirika ya upelelezi ya Marekani yanaamini kwamba mji mkuu wa Afghanistan, Kabul unaweza kuingia kwenye mikono ya Wataliban katika siku 90 zijazo.

 

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW