1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yapiga marufuku maandamano mjini Kabul

Sylvia Mwehozi
9 Septemba 2021

Maandamano yaliyopangwa kufanyika leo Alhamis mjini Kabul yamefutiliwa mbali baada ya kundi la Taliban kuyapiga marufuku na kuonya kuwa watakaokiuka agizo hilo watakabiliana na hatua kali za kisheria. 

Afghanistan Kabul | Demonstration gegen Pakistan
Picha: Hoshang Hashimi / AFP/Getty Images

Mapema wiki hii wapiganaji walio na silaha walitawanya mamia ya waandamanaji katika miji tofauti nchini Afghanistan ikiwemo mji mkuu wa Kabul, mji wa kaskazini mashariki wa Faizabad na ule wa magharibi wa Herat ambapo watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi.

Siku ya Jumatano Taliban iliazimia kuepusha machafuko zaidi ikisema maandamano yoyote yatahitaji kibali kwanza kutoka wizara ya sheria na kuongeza kwamba "kwa muda huu" hakuna maandamano yoyote yanayoruhusiwa.

Mapema Alhamis kulikuwa na ulinzi mkali wa Taliban kwenye mitaa ya mji wa Kabul huku wapiganaji walio na silaha wakifanya doria barabarani na vituo vya ukaguzi. Waandaaji wa maandamano wamelieleza shirika la habari la AFP kwamba wamefutilia mbali maandamano hayo kutokana na marufuku iliyotolewa usiku.

Hayo yakiendelea mamia ya raia wa kigeni wakiwemo Wamarekani wameondoka nchini humo leo kwa kutumia ndege za kibiashara kutokea uwanja wa ndege wa Kabul. Kuondoka kwa raia hao wa magharibi wapatao 200 kwa kutumia ndege za shirika la Qatar kuelekea Doha, kumeonyesha mafanikio ya uratibu baina ya Marekani na utawala mpya wa Taliban.

Ndege ya Qatar iliyoondoka na abiria wa kigeni waliosalia AfghanistanPicha: Wakil Kohsar/AFP

Taliban ilikuwa imeahidi kuwaruhusu wageni na Waafghani walio na vibali vya kusafiri kuondoka nchini humo, lakini mkwamo wa siku kadhaa juu ya ndege hizo za kibiashara katika uwanja mwingine wa ndege kuliibua wasiwasi wa utekelezaji wa zoezi hilo.

Wakati huohuo rais wa zamani wa Afghanistan Ashraf Ghani ambaye alikimbia nchi, ameomba msamaha kwa anguko la ghafla la serikali yake lakini akakana madai ya kwamba alikimbia na mamilioni ya dola. Katika taarfa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter, Ghani alisema kwamba aliondoka kutokana na ushauri wa timu yake ya usalama iliyomueleza kwamba endapo angesalia kungekuwa na kitisho cha "mapigano ya mtaani ya kutisha yaliyojitokeza wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 90".

"Kuondoka Kabul, ulikuwa moja ya uamuzi mgumu katika maisha yangu lakini niliamini kwamba ilikuwa njia pekee ya kunyamazisha silaha na kuiokoa Kabul na wakaazi wake milioni sita", ilisema taarifa ya Ghani. Kauli yake inashabiahana na ile aliyoitoa haraka wakati akiwa Umoja wa Falme za Kiarabu mara baada ya kukimbia nchi, hatua iliyokosolewa vikali na washirika wake wa zamani waliomtuhumu kwa usaliti.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW