1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yasherehekea kuondoka kwa Marekani

31 Agosti 2021

Kundi la Taliban linasherehekea kurejea tena madarakani kwa kuishinda Marekani baada ya vikosi vya mwisho vya Marekani kuondoka Afghanistan na kuvimaliza vita vilivyodumu kwa miongo miwili.

Afganistan, Flughafen in Kabul
Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Usiku wa Jumatatu majeshi ya Marekani yaliondoka katika uwanja wa ndege wa Kabul, ambako yalikuwa yakiendesha operesheni ya kuwaondoa watu kwa kutumia ndege na kufanikiwa kuwaondoa zaidi ya watu 130,000 walioukimbia utawala wa Taliban. Wwapiganaji wa Taliban waliokuwa na furaha waliingia kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamid Karzai na kufyatua risasi angani kama ishara ya kuchukua madaraka kamili.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid amewaambia waandishi habari kwamba ushindi huo ni wao wote na anawapongeza wananchi wote wa Afghanistan. Mujahid amesema ushindi huo ni funzo kwa wavamizi wengine.

''Kwanza nalipongeza taifa lote kwa sababu tumepata uhuru wetu na tumefanikiwa kuwalazimisha Wamarekani kuondoka. Baada ya miaka 20 ya vita vya jihadi na kujitoa, vikosi vyote vya kigeni, hasa Marekani vimeondoka Afghanistan jana usiku. Kwanza nataka kumshukuru Mungu aliyetupa rehema, na kisha nawashukuru wapiganaji wa Mujahideen na watu wote waliohusika katika harakati hizi na kujitolea,'' alifafanua Mujahid.

Hata hivyo, Taliban imerudia ahadi yake ya kuendesha serikali kwa kuvumiliana na kuwa wazi tofauti na utawala wake wa mwanzo uliokuwa wa mabavu. Mujahid amesema wanataka kuwa na uhusiano mzuri na Marekani na ulimwengu wote na kwamba wanakaribisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia. Aidha, amesisitiza kuwa wapiganaji wa vikosi vya usalama vya Taliban watakuwa wapole na wazuri.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah MujahidPicha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Wananchi wengi wa Afghanistan wana hofu kurudiwa kwa utawala wa awali wa Taliban uliodumua kuanzia mwaka 1996 hadi 2001, ambao ulikandamiza haki za msingi za wanawake na wasichana pamoja na kuwepo mfumo wa kikatili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ametangaza kuwa ubalozi wa Marekani umesitisha shughuli zake za kidiplomasia mjini Kabul na umehamishia shughuli zake Qatar. Blinken amesema kuna idadi ndogo ya raia wa Marekani waliobakia Afghanistan ambao ni takriban watu 100.

Utawala mpya utakuwaje

Macho yote sasa yameelekezwa katika utawala mpya wa Taliban kuangalia iwapo katika siku za mwanzo wataruhusu watu wanaotaka kuondoka, ikiwemo raia wa kigeni kufanya hivyo kwa uhuru. Maelfu ya Waafghani waliofanya kazi na serikali iliyokuwa inaungwa mkono na Marekani wanataka kuondoka wakihofia ulipizaji wa kisasi.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilipitisha azimio ambalo linaitaka Taliban kutimiza ahadi yake ya kuwaachia watu waondoke Afghanistan katika siku zijazo na kuruhusu uwepo wa Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kutoa misaada kuingia nchini humo.

Hata hivyo, azimio hilo halikuelezea kuhusu uwepo wa ''eneo salama'' wito uliotolewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Azimio hilo lililoandikwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa, limepitishwa kwa kuungwa mkono kwa kura 13 na hapakuwa na kipingamizi. China na Urusi zilijizuia kupiga kura.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Ahmad Al-Rubaye/AFP

Azimio hilo limesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kuwa Taliban itaruhusu kuondoka kwa usalama na mpangilio kwa raia wa Afghanistan na wale wa kigeni, kwa kuvuka mipaka kutumia njia za anga au ardhini.

Mazungumzo yanaendelea kwa sasa kuangalia nani atauendesha uwanja wa ndege wa Kabul. Taliban imeiomba Uturuki kusimamia vifaa, huku yenyewe ikidhibiti usalama, lakini Rais Recep Tayyip Erdogan bado hajaukubali wito huo. Bado haijafahamika wazi ni mashirika gani ya ndege yatakayokubali kuingia na kutoka Kabul.

Ujerumani yasubiri serikali mpya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema kuwa nchi yake inasubiri Taliban kutangaza serikali mpya kuangalia iwapo uongozi huo utaheshimu ahadi yake kuwaruhusu raia kuondoka Afghanistan kwa kutumia ndege katika uwanja wa Kabul. Kauli hiyo ameitoa Jumanne katika mkutano wa pamoja na waandishi habari mjini Islamabad na Waziri mwenzake wa Pakistan Shah Mehmood Qureshi.

Ama kwa upande mwingine, vikosi vya Taliban vimepambana na wanamgambo katika eneo la Panjshir kaskazini mwa Kabul Jumatatu usiku. Katika mapambano hayo wapiganaji wanane wa Taliban wameuawa.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW