1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yatangaza serikali mpya ya mpito Afghanistan

8 Septemba 2021

Taliban imetangaza serikali ya mpito ya Afghanistan. Veterani wa kundi hilo Mullah Mohammad Hassan Akhund ametangazwa mkuu wa serikali. Tangazo hilo limejiri wiki chache tangu Taliban ilipochukua madaraka kwa nguvu.

Afghanistan Kabul | PK der Taliban: Sprecher Zabihullah Mujahid: Mullah Mohammad Hasan Akhundzada soll Taliban leiten
Picha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Msemaji wa kundi hilo Zabiullah Mujahid amewaambia waandishi wa habari mjini Kabul kwamba Mullah Mohammad Hassan Akhund, ambaye alikuwa waziri wa ngazi ya juu katika utawala wa zamani wa Taliban uliojaa ukandamizi katika miaka ya 1990, ndiye ameteuliwa kuwa waziri mkuu.

Hassan Akhund ni miongoni mwa watu ambao wamewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa 

Kundi la Taliban liliahidi kuunda serikali itakayojumuisha kila jamii nchini humo, lakini nyadhifa zote za juu zimekabidhiwa viongozi wakuu wa vuguvugu hilo na mtandao wa Haqqani ambao ni tawi la Taliban na hufahamika kutokana mashambulizi yake ya kikatili.

Soma pia: Taliban yatangaza ushindi mkoa wa Panjshir

Katika orodha ya viongozi wa serikali waliotangazwa Jumanne hakuna mwanamke hata mmoja.

"Tutajaribu kujumuisha watu kutoka maeneo mengine ya nchi. Hii bado ni serikali ya mpito,” amesema Zabiullah Mujahid.

Muda mfupi tu baada ya majina ya maafisa wa serikali mpya kutangazwa, Hibatullah Akhundzada ambaye ni kiongozi mkuu wa Taliban ambaye hajawahi kuonekana hadharani, alitoa taarifa iliyoitaka serikali mpya kufanya bidi katika kuzingatia na kulinda sheria za Kiislamu na kutii Sharia.

Mullah Baradar Akhund ameteuliwa kuwa kaimu naibu wa waziri mkuu.Picha: SOCIAL MEDIA/REUTERS

Mullah Yaqoob ambaye ni mwanaye mwanzilishi wa kundi hilo ambaye pia alikuwa kiongozi mkuu marehemu Mullah Omar alitangazwa kuwa waziri wa Ulinzi, huku nafasi ya wizara ya mambo ya ndani ikikabidhiwa kwake Sirajuddin Haqqani ambaye ni kiongozi wa mtandao wa Haqqani.

Muasisi mwenza wa Taliban Abdul Ghani Baradar ambaye alisimamia utiaji saini wa makubaliano ya vikosi vya Marekani kujiondoa Afghanistan atakuwa naibu wa waziri mkuu.

"Si ajabu kwa njia yoyote kwamba serikali iliyotangazwa na Taliban haijawajumuisha Waafghani wote. Kundi hilo halikuwahi kudokeza kuwa baraza lake la mawaziri litajumuisha wasiokuwa watu wao," amesema Michael Kugelman ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kusini mwa bara Asia katika taasisi ya wasomi ya Woodrow Wilson.

Soma pia: Waafghani waandamana kupinga uingiliaji wa Pakistan

Lakini wakati Taliban linapojibadilisha kutoka kundi la kivita na kuwa kundi la kiutawala, maafisa wake wa usalama wanakabiliwa na ongezeko la maandamano yanayopinga utawala huo. Watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano hayo katika mji wa Heart magharibi mwa nchi hiyo.

Maandamano ya kupinga Taliban pia yanafanyika katika miji kadhaa nchini Afghanistan.Picha: Bilal Guler/AA/picture alliance

Hayo yanajiri mnamo wakati shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa OCHA, likitoa wito wa mchango wa dharura wa zaidi ya dola milioni 600 kusaidia katika utoaji misaada Afghanistan.

Msemaji wa shirika hilo Jens Laerke amesema huduma za msingi nchini Afghanistan zinaporomoka huku vyakula na misaada mingine ya kuokoa maisha ikikaribia kuisha.

Kulingana na Laerke, zaidi ya wanawake na watoto milioni moja nchini Afghanistan tayari wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri.

Soma pia: Ulaya wataja masharti ya kushirikiana na Taliban

Mashirika ya kutoa misaada yanatumai kuwa mchango utakaopatikana utawaepusha takriban watu milioni 11 dhidi ya njaa.

Mnamo Jumatatu, mratibu mkuu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alizuru Kabul kutathmini hali ilivyo mnamo wakati kuna hofu ya kutokea mgogoro wa kibinadamu.

Shirika la OCHA limetoa wito huo siku chache tu kabla ya mkutano utakaofanyika Jumatatu mjini Geneva utaongozwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu hali ya Afghanistan.

(AFPE, DPAE)