1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yawateua manaibu waziri

Bakari Ubena21 Septemba 2021

Viongozi wa Taliban wamewateua manaibu waziri katika utawala wao wa mpito na kutomteua hata mwanamke mmoja katika nyadhifa hizo licha ya malalamiko ya jumuiya ya kimataifa ya kutaka wanawake wapewe nafasi za uongozi.

Afghanistan Kabul Regierungsbildung Symbolbild
Picha: Bilal Guler/AA/picture alliance

Viongozi wa Taliban wamewateua leo manaibu waziri katika utawala wao wa mpito na kutomteua hata mwanamke mmoja katika nyadhifa hizo licha ya malalamiko ya jumuiya ya kimataifa ya kutaka wanawake wapewe nafasi za uongozi.

Ili kutuliza jazba hiyo, Taliban wamesema kuwa wasichana wameruhusiwa na wanatakiwa kurudi shule haraka iwezekanavyo. 

Afghanistan: Shule za sekondari zafunguliwa bila wasichana

Jumuiya ya kimataifa imeonya kuwa itawahukumu Taliban kutokana na matendo yao na jinsi kundi hilo litawatambua na kuwashughulikia wanawake na makundi ya watu wachache.

Katika uongozi wao wa awali nchini Afghanistan mwishoni mwa miaka ya 90, Taliban waliwatenga wanawake na wasichana katika maeneo mbalimbali ikiwa shuleni, kazini na hata kushiriki katika shughuli za umma.

Msuguano waongezeka kati ya pande mbili za uongozi wa Taliban

Siku ya Jumanne, Taliban walieleza kuwa, wameandaa sheria za kuwaruhusu wasichana na wanawake kurudi shuleni na hata kazini kwa kuzingatia sheria za Kiislamu, bila hata hivyo kufafanua zaidi ni lini hayo yatafanyika.

Wanajeshi wa Taliban wakishika doria mbele ya bango katika uwanja wa kimataifa wa ndege Kabul Septemba 9, 2021.Picha: WANA NEWS AGENCY via REUTERS

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid, ametetea uteuzi huo mpya mbele ya mkutano na wanahabari leo akisema kuwa, umewajumuisha wajumbe wa makabila ya walio wachache, kama wa Hazara na kwamba huenda wanawake wakaongezwa hapo baadae bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

"Ni jukumu la Umoja wa Mataifa pamoja na mataifa mengine kuitambua serikali yetu na kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na sisi," alisisitiza Mujahid.

Taliban wameunda baraza lao la mawaziri ambalo ndilo lenye majukumu yote ya kiserikali, lakini hawakueleza kama kutakuwepo na uchaguzi.

Afghanistan: Hofu yawaingia wafanyabiashara wa ususi Kabul

01:54

This browser does not support the video element.

Taliban wanalenga kupata msaada wa kimataifa wakati ambapo wanapambana na changamoto kuu ya kuliongoza taifa ambalo kwa miongo minne limekuwa likikumbwa na migogoro.

Taliban iliwaondoa viongozi wa nchi hiyo waliokuwa wakiungwa mkono na Marekani na walikuwa wakitegemea zaidi sana misaada kutoka nje.

Hata kabla ya kuchukua madaraka, uchumi wa Afghanistan ulikua katika hali mbaya ambayo kwa sasa inaendelea huku kukiwa na ongezeko la umasikini.

Hata hivyo, Mujahid ameonyesha kuwa nchi yake haina matatizo makubwa ya kiuchumi na kusema kuwa wananchi wa Afghanistan wana uwezo wa kuyatatua matatizo yao ya kiuchumi wenyewe ikiwa mapato ya ushuru yatakusanywa na kudhibitiwa vizuri.

Lakini, haijulikani ni vipi Taliban wanatarajia kukusanya mapato hayo, kwa raia ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 97 watakua wakiishi chini ya kiwango cha umaskini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

(AP, AFP)