1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Taliban yawazuia wanawake kujiunga na elimu ya juu

21 Desemba 2022

Utawala wa Taliban nchini Afghanistan umechukua uamuzi jana wa kuwazuia wanawake kote nchini humo kujiunga na vyuo vikuu.

Afghanistan Frauen Mädchen Schule
Picha: WAKIL KOHSAR/AFP

Serikali hiyo yenye msimamo mkali wa Kiislamu inaendelea kukiuka haki na uhuru wa wanawake ya kupata elimu.

Wanawake wamepigwa pia marufuku kutembelea sehemu za mapumziko pamoja na kumbi za michezo. Uamuzi huo umeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa iliyolaani vikali ukiukwaji huo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani uamuzi huo na kusema kuwa serikali ya Taliban inavunja ahadi yake ya kulegeza misimamo katika sheria zake.

Licha ya kuahidi kulegeza misimamo yake wakati walipoingia madarakani mwezi Julai mwaka jana, Taliban imeendelea kuimarisha vizuizi katika kila eneo linalohusu maisha ya mwanamke wa Afghanistan, huku wakipuuzilia mbali ukosoaji wa kimataifa.

Sehemu ya barua iliyosambazwa kwenye vyuo vikuu vyote vya serikali na binafsi na iliyosainiwa na waziri wa elimu ya juu Neda Mohammad Nadeem imesema "Mnaarifiwa kuanza mara moja utekelezaji wa agizo lililotajwa la kusitisha kuwaandikisha wanawake hadi kutakapotolewa tangazo jingine."