1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Taliban yazuia wanawake kujiunga na vyuo vikuu

21 Desemba 2022

Utawala wa Taliban nchini Afghanistan umetangaza kuwazuia wanawake kote nchini humo kujiunga na vyuo vikuu wakati serikali hiyo ya msimamo mkali wa Kiislamu ikiendelea kukiuka haki na uhuru wa wanawake. wa kupata elimu.

Afghanistan Kabul | Schule
Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Utawala wa Taliban nchini Afghanistan jana Jumanne umetangaza kuwazuia wanawake kote nchini humo kujiunga na vyuo vikuu, katika wakati ambapo serikali hiyo ya msimamo mkali wa Kiislamu ikiendelea kukiuka haki na uhuru wa wanawake wa kupata elimu. Agizo hili limeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa iliyolaani vikali ukiukwaji huo. 

Licha ya kuahidi kulegeza misimamo yake wakati walipoingia madarakani mwezi Julai mwaka jana, Taliban imeendelea kuimarisha vizuizi katika kila eneo linalohusu maisha ya mwanamke wa Afghanistan, huku wakipuuzilia mbali ukosoaji wa kimataifa.

Soma Zaidi: Mwaka mmoja wa Taliban madarakani

Sehemu ya barua iliyosambazwa kwenye vyuo vikuu vyote vya serikali na binafsi na iliyosainiwa na waziri wa elimu ya juu Neda Mohammad Nadeem imesema na hapa nanukuu "Mnaarifiwa kuanza mara moja utekelezaji wa agizo lililotajwa la kusitisha kuwaandikisha wanawake hadi kutakapotolewa tangazo jingine", mwisho wa nukuu.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema agizo hilo inaashiria kwa mara nyingine kwamba serikali ya Taliban inavunja ama kukiuka ahadi yake ya kulegeza misimamo. Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne mjini New York, Dujarric amerudia kusema kwamba ni ngumu kufikiria namna taifa hilo linavyoweza kuendelea na kupambana na changamotio zake bila ya kuwepo kwa ushiriki wa wanawake wasomi.

Amesema, "Ni nini hiki? ni wazi ahadi nyingine imevunjwa na Taliban. Tumeona tangu waliporejea madarakani miezi iliyopita, wanapunguza tu nafasi za wanawake, sio tu katika elimu, lakini hata kwenda kwenye maeneo ya umma na kutoshiriki katika mjadala wa umma. Ni hatua nyingine mbaya sana. Na ni vigumu kufikiria jinsi nchi inavyoweza kuendelea na inavyoweza kukabiliana na changamoto zake, bila ushiriki wa wanawake na elimu kwa wanawake."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amelaani hatua hiyo na kusema itakuwa na matokeo.Picha: Saul Loeb/AFP

Washington nayo imelaani vikali uamuzi huo, kwa kutoa matamko makali. Waziri wa mambo ya nje Anthony Blinken amesema kwenye taarifa yake kwamba Taliban wasitarajie kuwa mwanachama halali wa jamii ya kimataifa hadi pale itakapoamua kuheshimu haki ya raia wote wa Afghanistan na kuongeza kuwa uamuzi huo utakabiliwa na matokeo. Amesisitiza kwamba hakuna nchi itakayopiga hatua wakati nusu ya watu wake wanarudishwa nyuma.

Soma Zaidi: Taliban: yaweka zuio la kusafiri

Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Barbara Woodward amesema agizo hilo linaashiria hatua nyingine ya uminyaji mkubwa wa haki za wanawake, inayolizuia  taifa hilo kufikia uwezo wa kijitegemea.

Tangazo hili linatolewa chini ya miezi mitatu baada ya maelfu ya wasichana na wanawake kumaliza mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu kote nchini humo, wakati wengi wakiwa na ndoto ya kuwa walimu na madaktari iwapo wangejiunga na vyuo vikuu vitakavyofunguliwa mwezi Machi baada ya likizo ya majira ya baridi.

Baada ya Taliban kurejea mamlakani, vyuo vikuu vililazimishwa kutekeleza kanuni mpya ikiwa ni pamoja na kutenga madarasa kwa kuzingatia jinsia, na wanawake waliruhusiwa kufundishwa na maprofesa wanawake tu ama wanaume wazee.

Wasichana wengi tayari wamezuiwa kusoma elimu ya sekondari na hivyo kuwazuia moja kwa moja kujiunga na vyuo vikuu. Wengi wa wasichana hao walijikuta wakiolewa mapema na wanaume waliochaguliwa na baba zao. Familia nyingi zilizozungumza na shirika la habari la AFP mwezi uliopita zilisema ni bora kuwaoza ili kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi, kuliko kuwaacha bure nyumbani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW