1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha kubwa la Muziki dhidi ya Chuki dhidi ya Wageni

Oumilkheir Hamidou
4 Septemba 2018

Tamasha kubwa la muziki dhidi ya hisia za chuki na ubaguzi dhidi ya wageni, na vurugu nchini Libya ni miongoni mwa mada magazetini.

Deutschland, Chemnitz: Konzert gegen Rassismus
Picha: picture alliance/dpa/J. Stratenschulte

Tunaanzia Chemnitz, katika jimbo la Saxony ambako jana usiku makundi mashuhuri ya wanamuziki wa jimbo hilo na kwengineko nchini Ujerumani yaliandaa tamasha kubwa la muziki dhidi ya hisia za chuki na ubaguzi dhidi ya wageni. Zaidi ya watu 65, 000 walihudhuria tamasha hilo, kauli mbiu ikiwa "Wir sind Mehr", yaani sisi ndio wengi zaidi. Maandamano yamepita salama lakini wahariri wanakubaliana ufumbuzi dhidi ya siasa kali za mrengo bado haujapatikana. Gazeti la "Sächsische Zeitung" la mjini Dresden" linaandika:"Suala kubwa hapa ni jee kipi kitafuatia mdundo wa mwisho? Wanazi mambo leo hawatishiki hata kidogo kwa muziki  wa makundi ya mrengo wa kushoto, ya Rock, Rap, Punk au Reggaie. Na wengine pia wanaoshuku kama juhudi za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii zitafanikiwa, shaka shaka zao hazikubadilika. Ufa hauigawi pekee jamii ya wakaazi wa Saxony. Na wanamuziki, licha ya dhamiri yao nzuri na matamshi ya kuaminika jukwaani na kwengineko, hawatoweza kuufunika."

Wanaasiasa wasikilize na kuzingatia malalamiko ya wananchi

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" la mjini Chemnitz anazungumzia kasoro zilizoko katika sera ya wahamiaji na kuandika: Ndio kuna kasoro bayana na makosa yaliyotokea katika sera ya wakimbizi. Hilo hakuna anayelibisha. Hata hivyo, kuangalia yaliyopita peke yake haisaidii kitu, badala yake inawapa nguvu wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Muhimu zaidi ni kujifunza kutokana na makosa yote yaliyotokea na hilo linapindukia makosa ambayo tayari yameshasawazishwa katika sera ya wakimbizi. Nafasi sawa, nyumba za bei ya wastani, kazi za mishahara ya haki, malipo tosha ya uzeeni, uwanja mpana wa mafunzo, huduma bora za afya, yote hayo ni muhimu ikiwa tunataka kuhakikisha usalama katika jamii na kuwalinda dhidi ya hisia kali za kizalendo. Na bila ya shaka panahitajika taifa lenye nguvu na wanasiasa wanaojali na kusikiliza matatizo ya wananchi pamoja na raia wanaoonesha moyo wa kijasiri."

Libya inayohitaji kusaidiwa, haiwezi kusaidia

Hali nchini Libya nayo pia imechambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Kuhusu vurugu zinazoendelea nchini humo, gazeti la "Oberhessische Presse" linaandika: "Si ajabu kama walinzi wa jela mjini Tripoli wanawafungulia milango wafungwa 400 waliokuwa wakifanya fujo, ili kuyanusuru maisha yao. Si ajabu pia kwamba katika mwambao wa Libya makundi ya wenye kusafirisha watu kinyume na sheria wanaendelea na vituko vyao bila ya kuhofia polisi wala walinzi wa fukwe. Katika nchi ambayo ulimwengu mzima unashuhudia jinsi inavyozama katika bahari ya vurugu, vikosi vya usalama vinajishughulisha zaidi na hatima yao badala ya kuwazuwia watu wasiyatose maisha yao baharini. Libya, kutokana na hali namna ilivyo hivi sasa si mshirika wa kuaminika wa Ulaya katika masuala ya wakimbizi na wahamiaji. Libya haiwezi kuisaidia Ulaya. Libya binafsi inahitaji kusaidiwa.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef