Tamasha la mwanamuziki Fally Ipupa laua watu 11 Kinshasa
30 Oktoba 2022Watu 11 wamefariki jumamosi wakiwemo maafisa wawili wa polisi katika mkanyagano kwenye uwanja wa michezo uliokuwa umefurika watu waliokwenda kuhudhuria tamasha mjini Kinshasa.
Uwanja wa mashahidi ulisheheni kupita kiwango kinachotakiwa ambapo watu 80,000 walioujaza uwanja huo kwa ajili ya kushuhudia tamasha la mwanamuziki wa Kongo Fally Ipupa,kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani.
Waandishi habari wa Reuters wamefahamisha kwamba baadhi ya mashabiki wengine walijilazimisha kuingia kwenye eneo la watu maalum yaani VIP na maeneo mengine maalum yaliyotengwa katika uwanja huo.
Taarifa ya polisi imeonesha watu 11 wamefariki kutokana na kukosa hewa pamoja na mkanyagano na wengine 7 wamelazwa hospitali kwa mujibu wa tamko lililotolewa na waziri wa mambo ya ndani wa Kongo Daniel Aelo Okito.
Imeelezwa kwamba awali polisi walitumia gesi ya kutowa machozi katika jitihada ya kuwatawanya watu waliokuwa wakifanya vurugu katika barabara za nje ya uwanja huo ambako watu walikuwa wameshakusanyika kabla ya tamasha hilo la mwanamuziki mzaliwa wa Kinshasa Fally Ipupa.
Mwanamuziki huyo amejipatia umarufu mkubwa ndani ya Kongo ,ulaya na kwengineko. Idadi ya walioujaza uwanja ilikuwa imepindukia kiasi ambacho kinaweza kudhibitiwa na walinda usalama wa serikali na wale wa kibinafsi waliokuweko.