1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la utalii lafunguliwa Nairobi

Thelma Mwadzaya3 Oktoba 2018

Tamasha la kimataifa la Utalii limefunguliwa rasmi jijini Nairobi. Zaidi ya mataifa 30 yanawakilishwa katika maonyesho ya Magical Kenya yatakayoendelea hadi mwishoni mwa wiki

Nairobi Skyline Kenia Zebras
Picha: Getty Images

Tamasha la Utalii la kimataifa linafunguliwa rasmi hii leo jijini Nairobi pembezoni mwa kongamano la wawekezaji wa utalii na maonyesho ya usafiri ya Kenya. Tamasha hili linafanyika ikiwa imepita wiki moja tangu siku ya kimataifa ya utalii kuadhimishwa kote ulimwenguni.Kauli mbiu ya siku hiyo ilijikita katika matumizi ya teknolojia na mifumo ya dijitali kuimarisha biashara ya utalii katika Nyanja zote.

Tamasha la Utalii limefunguliwa rasmi kwenye ukumbi wa mikutano na maonyesho ya kimataifa wa KICC ulioko katikati ya jiji la Nairobi. Zaidi ya mataifa 30 yanawakilishwa katika maonyesho ya 8 ya usafiri na utalii ya Magical Kenya yatakayoendelea hadi mwishoni mwa wiki hii. Waziri wa Utalii wa Kenya Najib Balala alisisitiza kuwa mambo yanaendelea kuimarika katika hotuba yake ufunguzi.

Wageni wengi wanatokea Ulaya, Asia, Marekani na Afrika yenyewe. Katibu Mkuu wA shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Zurab Polilishkavili ameeleza imani kuwa tamasha hili na maonyesho litaiweka Kenya na bara la Afrika kwenye nafasi nzuri zaidi ya kunadi bidhaa zake.

Ajenda kuu ni kulinadi bara la Afrika katika biashara ya utalii.

Kongamano la wawekezaji linaendelea katika hoteli ya Radisson Blu iliyoko eneo la Upperhill jijini Nairobi na kikao cha mawaziri wa utalii wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika kimekamilika jijini Nairobi. Ajenda kuu ni kulinadi bara la Afrika katika biashara ya utalii.

Waandalizi wamesema tamasha hilo na maonyesho kwa pamoja yataiweka Kenya na bara la Afrika kwenye nafasi nzuri zaidi ya kunadi bidhaa zake.Picha: PHIL MOORE/AFP/Getty Images

Wiki iliyopita ulimwengu uliadhimisha siku ya kimataifa ya Utalii ambayo kauli mbiu yake ilijikita katika matumizi ya mifumo ya dijitali kuimarisha biashara na uwekezaji katika nyanja zote katika muktadha wa mawasiliano, utoaji wa huduma na kutangaza bidhaa.

Kwenye kongamano la wawekezaji, wadau wamekiri kuwa mambo yamekuwa magumu zaidi kufanya biashara ya hoteli za kifahari katika eneo lililo kusini mwa jangwa la sahara ila mustakabal unaleta matumaini. Kwa mara ya kwanza wameibuka wamiliki wa maboti ya kifahari yanayowasafirisha wageni kutokea Tanzania hadi kisiwa cha Ushelisheli kadhalika kuandaa maonyesho ya Utalii ya Site yatakayofanyika jijini Dar es Salaam.

Maonyesho ya utalii na usafiri ya Magical Kenya ndio makubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki yanayowapa wafanyabiashara wa afrika kwa jumla fursa ya kukutana ana kwa ana na kubadilishana mawazo vilevile kunadi bidhaa zao kwa lengo la kupata masoko na wateja wapya.Tamasha la utalii la kimataifa litahitimishwa Ijumaa wiki hii.Kutoka Nairobi mimi ni TM,DW.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga