1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamko la jeshi la Myanmar lapunguza hofu ya mapinduzi

Yusra Buwayhid
30 Januari 2021

Jeshi la Myanmar limesema litailinda na kuifuta katiba ya nchi, tamko lilopunguza wasiwasi wa jeshi hilo kujaribu kufanya mapinduzi. Jeshi limekuwa likidai kuwa uchaguzi wa Novemba 2020 ulikuwa na undanganyifu.

Myanmar Wahlen Sicherheitskräfte
Picha: Thet Aung/AFP

Tamko hilo la Jumamosi limetolewa siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na balozi za mataifa ya Magharibi nchini Myanmmar kugusia uwezekano wa kuingilia kati Mnyanmar kijeshi. Myanmar imekuwa ikiongozwa na jeshi kwa miaka 49, tangu baada ya mapinduzi ya mwaka 1962.

Jeshi la Myanmar linalojulikana kama Tatmadaw limesema hivi karibuni kwamba taarifa ya mkuu wa majeshi jenerali Min Aung Hlaing, kuhusu kuondoa katiba ya nchi imeeleweka vibaya.

"Jeshi la Tatmadaw linalinda katiba ya 2008 na linafanya kazi kulingana na sheria," ilisema taarifa hiyo." Baadhi ya vyombo vya habari vilifahamu kauli hiyo vibaya na kuandika kwamba Tatmadaw linataka kuondosha katiba. "

Chama cha Aung San Suu Kyi cha National League for Democracy (NLD), kilichoshinda kwa kishindo uchaguzi uliopita wa Novemba, kimelieleza tamko hilo la jeshi kuwa ni "maelezo yanayofaa."

Msemaji wa NLD Myo Nyunt ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba chama kimelitaka jeshi kukubali chaguo la wananchi katika uchaguzi huo.

Mchambuzi wa siasa Myanmar Richard Horsey amesema kwa sasa hakuna tena kitisho cha kufanyika mapinduzi ya kijeshi.

"Inavyoonyesha jeshi la Myanmar limerudi nyuma baada ya kutishia kufanya mapinduzi," ameandika Horsey kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mivutano ya kisiasa ilipamba moto wiki hii pale msemaji wa jeshi alipokataa kurudi nyuma kufanya mapinduzi kabla ya kikao cha kwanza cha bunge wiki ijayo, na kuonya kwamba vikosi vya usalama vitachukua udhibiti wa nchi iwapo malalamiko ya wizi wa kura hayatoshugulikiwa ipasavyo.

Wananchi waandamana kuliunga mkono jeshi

Maandamano ya kuunga mkono msimamo wa jeshi yalifanywa katika miji mikubwa kadhaa nchini humo. Jumamosi, watu wapatao 200 waliandamana katika jiji la kibiashara Yangon, wakipinga uingiliaji kati wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchini Myanmar.

Aung San Suu Kyi akipiga kura wakati wa uchaguziPicha: Aung Shine Oo/AP Photo/picture alliance

Kundi hilo la waandamanaji linaitaka serikali na tume ya uchaguzi kushughulikia malalamiko ya kutokea udanganyifu wakati wa uchaguzi.

Soma zaidi: Myanmar yawaachia waandishi wa Reuters

Tume ya uchaguzi Alhamisi ilikataa madai ya jeshi ya ulaghai wa kura, ikisema hakukuwa na makosa makubwa ya kuweza kuutilia shaka uhalali wa uchaguzi.

Tangu kumalizika uchaguzi, mara kadhaa jeshi limelalamika kufanyika makosa wakati wa uchaguzi, ambao ulikipa ushindi chama cha NLD na kuweza kunyakua asilimia 83 ya viti bungeni. Tangu ushindi huo kutangazwa, kumekuwepo mivutani isiyowahi kushuhudiwa kati ya serikali na jeshi la Myanmar. Pande hizo mbili kwa kawaida zinagawana madaraka ya kuliongoza taifa hilo la Kusini-Mashariki mwa Asia.

Kulingana na katiba ya nchi, jeshi la Myanmar linastahili kupewa asilimia 25 ya viti bungeni pamoja na udhibiti wa wizara tatu muhimu katika serikali ya Suu Kyi.

Thant Myint-U, mwanahistoria na mwandishi wa kitabu, "The Hidden History of Burma" amesema kilicho muhimu hivi sasa ni kuhakikisha taifa hilo linapata demokrasia. "Lakini muhimu pia ni kupata suluhisho la mgogoro wa sasa ambalo halitadhuru matarajio ya kupata amani nchini humo," Myint-U aliiambia shirika la habari la AFP.

Vyanzo: (afp,rtre,)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW