1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamko la Mori lamtia matatani

11 Februari 2021

Rais wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Tokyo Yoshiro Mori anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kutokana na matamshi yake kwamba wanawake huzungumza sana katika mikutano.

Japan | Yoshiro Mori | Vorsitzender olympisches Organisationskomitee
Picha: Kim Kyung-hoon/AP Photo/picture alliance

Rais wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Tokyo Yoshiro Mori anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu baada ya kuzua hasira ya umma nchini Japan na sehemu nyingine duniani kutokana na matamshi yake kwamba wanawake huzungumza sana katika mikutano.

Uamuzi huo unakuja baada ya Rais huyo wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Tokyo kukosolewa vikali kuanzia na wanasiasa hadi wanamichezo kote duniani.

Tamko hilo la Mori kuwa wanawake huzungumza sana katika mikutano linaonekana kuwa kizingiti kingine cha karibuni kwa waandalizi wa michezo hiyo ya Olimpiki hasa katika wakati huu ambapo wanakabiliwa na shinikizo la umma juu ya uamuzi wao wa kuendelea na mipango ya kuandaa michezo ya Olimpiki ya msimu wa joto licha ya janga la virusi vya corona.

 Mrithi wake anatajwa kuwa Saburo Kawabuchi

Vyombo kadhaa vya habari nchini Japan, vikinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa wazi, vimeripoti kuwa Mori mwenye umri wa miaka 83 amewaambia maafisa kuwa ananuia kujiuzulu na atatangaza hatua hiyo katika mkutano na waandalizi wa michezo hiyo mnamo siku ya Ijumaa.

Mori alisema " unapoongeza idadi ya wajumbe waandamizi wa kike, kama muda wa kuzungumza hautawekewa ukomo, inakuwa ngumu kwao kumaliza, kitu ambacho kinakera," alisema.

Hata hivyo, ameomba radhi kutokana na matamshi hayo yanayodaiwa kuwa yamewadhalilisha wanawake, huku akisisitiza kwamba anarudia tu yale yanayosemwa na wengine, lakini aliongezea kadhia hiyo pale alipoeleza kwamba "huwa sizungumzi sana na wanawake."

Vyombo vya habari vya Japan vimeripoti kuwa nafasi yake huenda ikachukuliwa na Saburo Kawabuchi, msimamzi wa michezo wa muda mrefu, ambaye inasemekana amekubaliana na ombi hilo.

Mori ambaye ni waziri mkuu wa zamani, amekabiliwa na shinikizo kubwa tangu alipotoa matamshi hayo mbele ya wajumbe wa kamati ya Olimpiki ya Japan wiki iliyopita.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW