1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: CHADEMA yaanza kupokea ruzuku ya serikali

7 Machi 2023

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kinaonekana kuingia katika mkanganyiko kuhusu hatua yake ya kuanza kupokea ruzuku ya serikali hatua ambayo inakinzana na msimamo wake wa awali wa kugomea ruzuku hiyo.

Chadema Chairman Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema kuwa kimeanza kupokea ruzuku hiyo hivi karibuni ingawa baadhi ya viongozi wake wakuu wamekuwa wazito wa kutoa taarifa za moja kwa moja licha kwamba duru kadhaa kubainisha juu ya ukweli wa jambo hilo.

Chadema ilisusia ruzuku hiyo kwa madai ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 kuvurugwa kwa lengo la kupendelea upande mmoja wa siasa, huku pia ikosoa vikali kitendo cha waliokuwa wanachama wake 19 wanawake kuingizwa bungeni kinyemela bila ridhaa ya chama.

Soma pia: Tundu Lissu na harakati za "mwanzo mpya" Tanzania

Lakini sasa kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa chama hicho, wamekuwa wakitupiana mpira kutoa kauli ya moja kwa moja iwapo kama imebadili msimamo au la.

Kwa kauli yake, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anataka suala hilo litupwe kwa katibu wake mkuu, John Mnyika ambaye naye hata hivyo, ameonyesha kutokuwa tayari kubainisha ukweli wa mambo.

Hata hivyo, makamu mwenyekiti Tanzania bara, Tundu Lissu amefichua ukweli wa mambo akisema hama hicho kimeanza kupokea ruzuku hiyo.

Lissu aliyerejea ughaibuni kwa muda na wakati akishiriki mjadala mmoja kwenye mtandao wa Club House alidokeza juu ya sula hilo akisema Chadema wameanza kupokea kiasi fulani cha fedha kama ruzuku.

Makamu mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania bara, Tundu LissuPicha: Eric Boniface

Kumekuwa na maoni mseto kuhusiana na hatua ya chama hicho ambacho bado kinaendelea na ajenda yake ya kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Baadhi wanaona hatua yake ya kuelekea kule ilikokupinga imesukumwa na mwelekeo mpya wa kisiasa unachukuliwa na serikali ya awamu ya sita inayohimiza mshikamano na maridhiano ya pamoja. 

Soma pia: Rais Samia asema yuko tayari kuvumilia na kusamehe

Kwa muda kwa miezi kadhaa sasa viongizi wa chama hicho kikuu cha upinzani na wale wa chama tawala CCM wamekuwa wakikaribiana mara kwa mara katika kile kinachotajwa ni daraja la kujenga maridhiano ya kisiasa.

Na chama hicho kinatarajia kumkaribisha Rais Samia Suhulu Hassan katika jukwaa lake wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanayofanyika kesho Machi Nane.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW